Na Muhidin Amri, Namtumbo
SERIKALI imesema,ujenzi wa Barabara ya Lumecha-Kitanda-Londo-Malinyi inayounganisha Mkoa wa Ruvuma na Morogoro kwa kiwango cha lami utaanza mwaka huu wa fedha 2026/2027.
Kauli hiyo ya SERIKALI imetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria DKT Juma Homera,amesema hayo Jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa vijiji vya Mputa,Naikesi na Kitanda wilaya ya Namtumbo wakati wa ziara yake kusikiliza kero na kukagua shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wananchi wilayani Namtumbo.
Alisema,serikali tayari imempata mkandarasi kampuni ya China Civil Engneering Co Ltd itakayojenga barabara hiyo ili kurahisisha usafiri,biashara na kufungua fursa mpya za kiuchumi,kijamii na maendeleo kwa mikoa yote miwili na Taifa kwa ujumla.
“,Awali mkandarasi alipatikana lakini hakuwa na mtaji,hivyo alishindwa kuanza ujenzi wa barabara hii,lakini sasa Serikali imeamua kujenga kwa fedha zake zenyewe badala ya kusubiri fedha za wafadhili,dhamira ya Serikali ni kuwekeza kwenye mundombinu ili kuunganisha watu na kuongeza uchumi na kuimarisha ushindani wa kitaifa na kimataifa”alisema Dkt Homera.
Hata hivyo baadhi ya ya wakazi wa kijiji cha Kitanda,wameiomba Serikali kupitia wizara ya ujenzi kuharakisha mchakato wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Wamesema,barabara hiyo muhimu kiuchumi kwani itaunganisha vijiji vilivyopo katika wilaya ya Namtumbo na wilaya jirani ya Kilosa mkoa wa Morogoro,hivyo kutoa fursa kubwa kufanya biashara mbalimbali ikiwemo mazao na uvuvi.
Hassan Nyoni alisema,kwa muda mrefu barabara hiyo inatajwa kila inapofika muda wa uchaguzi, lakini baada ya uchaguzi kumalizika hakuna utekelezaji wake hivyo wananchi wanaendelea kuteseka kwa kukosa mawasiliano ya uhakika hasa wanapohitaji kusafirisha mazao.
Alisema,barabara ya Lumecha-Kitanda-Londo ni fupi kwenda mikoa ya Morogoro na D,slaam,hata hivyo kwa kuwa bado haijajengwa kwa lami au kuboreshwa kwa changarawe ni vigumu kupita wanapotaka kwenda mikoa hiyo kwa ajili ya kufanya biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.
John Ngonyani alisema,kwa muda mrefu sasa barabara hiyo inahaidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami na viongozi wa kisiasa na serikali hasa wa wizara ya ujenzi,lakini hadi sasa hakuna ukweli wa kauli zao huku wananchi wanaendelea kuteseka.
