Wakili wa Serikali wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Tamari Z. Mndeme, ameongoza kikao cha Kamati ya Ushauri wa Kisheria cha Mkoa kilichofanyika tarehe 13 Agosti 2026 katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa.
Kikao kazi hicho kilikuwa kilichokiwa na agenda kuu mbili ambazo ni Kupanga mpango mkakati ya utekelezaji wa majukumu ya kamati hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027, pamoja na kusikiliza na kupata utatuzi wa mashauri matatu ya wananchi yaliyowasilishwa mbele ya Kamati.
Katika kikao hicho kamati ilisikiliza Mgogoro wa Wananchi 158 kutoka (Hai) dhidi ya Kampuni ya SAORE Limited, ambapo juhudi za kamati kusuluhisha suala hilo hazikufanikiwa, hivyo Kamati ilishauri shauri hilo lifunguliwe rasmi katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya Kampuni ya SAORE Limited.
Aidha, Kamati hiyo ilisikiliza mgogoro wa Ardhi wa Rau Sabasaba dhidi ya Mwekezaji, ambao umedumu kwa miaka 8, na na baada ya mahojiano, pande zote mbili ziliahirisha kikao hadi tarehe nyingine ili kumpa nafasi Afisa Ardhi Mteule na Mipango Miji kupitia kumbukumbu za ofisi na kuwasilisha majibu rasmi mbele ya kamati katika kikao kijacho ili haki ipatikane.
Sambamba na hilo, Kamati ya Ushauri wa Kisheria mkoa wa Kilimanjaro ilisikiliza pia mgogoro wa Ardhi wa Kanisa la Nkuu Lutheran Moshi dhidi ya Wananchi, ambapo Usuluhishi wa shauri hilo haukuweza kukamilika kufuatia Mchungaji Kiongozi (kama mwakilishi wa kanisa) kushindwa kuhudhuria kwasababu zilizokuwa nje ya uwezo wake.
Katika hatua nyingine Wakili wa Serikali Bi. Tamari Mndeme aliwaagiza maafisa kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi kuandaa na kuwasilisha ripoti inayotakiwa mapema iwezekanavyo ili kuharakisha upatikanaji wa haki na kurudisha tabasamu kwa wananchi.
Vilevile, Bi. Mndeme aliwasihi wananchi kujenga utamaduni wa kufika kwenye vyombo rasmi vya kisheria na utoaji haki pindi wanapokutana na changamoto, badala ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari kabla ya kutumia misingi ya kisheria iliyopo.

