▪️Ni kupitia Local Content
▪️ Yatenga Huduma na Bidhaa 20 kwa ajili ya Kampuni za kitanzania pekee
▪️ Watanzania wanufaika asilimia 86 ya manunuzi ya bidhaa na huduma migodini
▪️ Ajira 20,421 zazalishwa, Watanzania wachukua asilimia 94
📍DODOMA
Serikali imeendelea kufanya maboresho katika Sheria na Kanuni za Madini kwa lengo la kuongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini, hususan katika utoaji wa huduma, usambazaji wa bidhaa na upatikanaji wa ajira migodini.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati akitoa ufafanuzi kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini leo Agosti 14, 2026 Bungeni jijini Dodoma waliotaka kujua ni namna gani Serikali imejipanga kutekeleza mpango wa Uwajibikaji wa Wamiliki wa Leseni kwa Jamii na Ushirikishwaji wa Watanzania katika Uchumi wa Madini.
Amesema kuwa, kupitia Tume ya Madini, Serikali imetenga bidhaa na huduma 20 zinazopaswa kusambazwa na kutolewa na Watanzania au kampuni zinazomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100, hatua inayolenga kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini na kunufaika na fursa zinazotokana na uwekezaji huo.
Waziri Mavunde ameongeza kwamba, takwimu zinaonesha kuwa hadi Juni 2026, jumla ya ajira 20,421 zilikuwa zimezalishwa katika migodi mbalimbali nchini, ambapo Watanzania walikuwa wameajiriwa 19,690, sawa na asilimia 94 ya ajira zote.
Aidha, ameleza kwamba kampuni za madini zilitumia jumla ya Sh trilioni 5.2 kununua bidhaa na huduma, ambapo Sh trilioni 4.4, sawa na asilimia 86, zilitumika kununua bidhaa na huduma kutoka kampuni za Kitanzania, huku Sh bilioni 727.2, sawa na asilimia 14, zikitumika kwa kampuni za kigeni.
Katika eneo la uwajibikaji kwa jamii (CSR), Waziri Mavunde amesema katika Mwaka wa Fedha 2025/26, wamiliki wa leseni za madini walitumia takribani Sh bilioni 25.4 kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri zinazozunguka maeneo ya uchimbaji wa madini.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo na kuhakikisha kampuni zinazomiliki leseni za madini zinazingatia matakwa ya kisheria ya kununua bidhaa na huduma zinazopatikana nchini, huku watoa huduma wakitakiwa kuhakikisha bidhaa na huduma zao zinaendana na viwango vinavyohitajika migodini.
Sambamba na hayo, Waziri Mavunde amesema, Wizara ya Madini imeanza kutekeleza mpango wa Mining For A Brighter Tomorrow (MBT) kwa lengo la kuongeza ushiriki wa vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum katika mnyororo wa thamani wa madini. Kupitia mpango huo, maeneo yenye taarifa za kijiolojia yametengwa kwa ajili ya kutolewa leseni kwa makundi hayo ambapo hadi sasa, mpango wa MBT umewezesha kutolewa kwa jumla ya leseni 273 kwa vikundi 183, vyenye wanufaika 2,550 katika mikoa mbalimbali nchini.
Aidha, Waziri Mavunde ametoa maelekezo kwa Maafisa Madini nchi nzima kwamba hakuna kutoa leseni ya uchimbaji bila kujiridhisha kama kuna shughuli za uchimbaji zinazoendelea katika husika ili kuepusha migogoro katika maeneo ya uchimbaji.
Pia, Waziri Mavunde ameishukuru Kamati hiyo kwa usimamizi, ushauri na maelekezo ya kamati hiyo ambapo pia ameahidi kuendelea kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Kamati hiyo sambamba na kuweka mikakati ya kuijengea uwezo Kamati hiyo kwa ajili ya kuongeza uelewa wa wajumbe wa Kamati hiyo kwenye sekta ya madini.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mh. Simon Songe ameitaka Serikali kuhakikisha watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye mnyororo mzima wa sekta ya madini ili kuacha manufaa makubwa nchini ya kuongezeka kwa mapato na ajira.

