NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amezindua Kliniki ya Watumishi wa Umma inayolenga kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili watumishi na wastaafu katika Mkoa wa Iringa, akisisitiza kuwa utatuzi wa changamoto za watumishi ni msingi wa kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kliniki hiyo uliofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma kupitia maboresho ya mishahara, upandishaji wa madaraja, ajira mpya na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa rasilimali watu.

Alisema pamoja na hatua hizo, bado zipo changamoto zinazowakabili baadhi ya watumishi na wastaafu, ikiwemo malimbikizo ya mishahara, madai ya likizo, uhamisho, matibabu, kupandishwa madaraja, mafao ya wastaafu pamoja na fidia kwa watumishi wanaoumia kazini.

“Lengo la kliniki hii siyo kutafuta makosa ya watu, bali kutafuta suluhisho la madai, manung’uniko na changamoto za watumishi na wastaafu ili wafanye kazi wakiwa na utulivu wa akili, motisha na imani kuwa haki zao zinapatikana pale inapostahili,” alisema Kheri.

Amesema kliniki hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuwafikia watumishi walipo badala ya kuwalazimisha kutumia muda na fedha kusafiri kwenda maeneo mbalimbali kufuatilia changamoto ambazo zinaweza kutatuliwa ndani ya mkoa.

Kheri alisema kuwa mpango huo ni muhimu hasa kwa watumishi wanaotoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi, wakiwemo madaktari, walimu na watumishi wengine, ambao wanapokuwa na changamoto zisizotatuliwa wanaweza kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi unaotarajiwa.

“Tunataka watumishi wetu wafanye kazi wakiwa na furaha na utulivu tunatatua changamoto za watu wetu ili nao wakaweze kutatua changamoto za wananchi wenzao,” amesema.

Ameongeza kuwa kliniki hiyo itasaidia pia kupunguza muda na gharama ambazo watumishi wamekuwa wakitumia kufuatilia masuala yao katika taasisi za Serikali zilizopo nje ya mkoa

“Yawezekana mwalimu ana jambo linaloweza kushughulikiwa na Ofisi ya Utumishi ya Mkoa au Wilaya, lakini akalazimika kusafiri hadi TAMISEMI au Utumishi hivyo hii kliniki inarahisisha jambo hilo kushughulikiwa hapa hapa Iringa,” amesema.

Kheri pia amewataka viongozi na wataalamu wanaoshiriki katika kliniki hiyo kutoa huduma kwa weledi, uadilifu na heshima, kusikiliza kila mtumishi na mstaafu bila ubaguzi na kutoa majibu yanayozingatia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali.

Amesisitiza kuwa pale ambapo suala haliwezi kutatuliwa papo hapo, mtumishi apewe mrejesho wa hatua zitakazochukuliwa pamoja na muda wa utekelezaji, huku akitaka hakuna changamoto inayopuuzwa au kuachwa bila kufuatiliwa.

Aidha amesema ustawi wa watumishi unapaswa kwenda sambamba na ustawi wa wananchi, akieleza kuwa Serikali inapoboresha mishahara, madaraja na mazingira ya kazi, watumishi nao wanapaswa kulipa kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Serikali imeshughulika na madaraja, mishahara na maeneo mazuri ya kufanya kazi sisi jitihada hiyo inayofanywa na Serikali lazima tuitafsiri kwa huduma bora kwa wananchi. Ustawi wa watumishi uende sambamba na ustawi wa wananchi,” amesema Kheri.
Kliniki hiyo inafanyika kuanzia Agosti 13 hadi 20, 2026, katika halmashauri zote tano za Mkoa wa Iringa, ambapo watumishi na wastaafu watapata fursa ya kuwasilisha changamoto zao na kupata ufumbuzi au maelekezo ya namna ya kuzifanyia kazi.

Kwa upande wake, Nuru Sobela, ambaye ni mratibu wa Kliniki ya Watumishi wa Umma Mkoa wa Iringa na Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Utumishi na Usimamizi wa Rasilimali Watu, amesema kliniki hiyo imeandaliwa kwa ajili ya kusikiliza kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa umma.

Amesema katika kliniki hiyo yameandaliwa madawati mbalimbali, ikiwemo dawati la mfumo, mishahara, masuala ya watumishi wanaoumia kazini pamoja na dawati maalum kwa ajili ya wastaafu.

Ameeleza kuwa dawati la wastaafu linafanya kazi kwa kushirikiana na PSSSF ili kuhakikisha changamoto za wastaafu zinapatiwa ufumbuzi.
Mbali na masuala ya utumishi, amesema taasisi mbalimbali zimeungana na zoezi hilo kutoa huduma kwa watumishi, zikiwemo NHIF, NIDA na taasisi za benki.

Nuru amewataka watumishi wote wa umma katika Mkoa wa Iringa kutumia fursa hiyo kufikisha changamoto zao ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.

Amesema baada ya uzinduzi wa kliniki hiyo katika makao makuu ya mkoa, zoezi litaendelea katika maeneo mengine, ambapo tarehe 17 na 18 Agosti litafanyika Wilaya ya Kilolo, huku tarehe 19 na 20 Agosti likifanyika Wilaya ya Mufindi.

Amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mtumishi anapata mazingira rafiki ya kuwasilisha hoja zake, kufuatilia haki zake na kupata majibu bila kutumia gharama kubwa au muda mwingi wa kuacha kituo chake cha kazi.