Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, Wazo Mwang’onda, akikata utepe kuzindua mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji wa Igombe-Kabangaja, wilayani Ilemela, leo.

Msimamizi wa Mradi wa MWAUWASA, Mhandisi Nuhu Said (kulia), akitoa taarifa  kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, Wazo Mwang’onda (wa pili kutoka kulia), kuhusu mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji wa Igombe-Kabangaja, wilayani Ilemela, leo.

Mwenge wa Uhuru ukiwa eneo la mradi wa kuchuja maji wa Igombe-Kabangaja, leo.

Picha zote na Baltazar Mashaka

………..

NA BALTAZAR MASHAKA, ILEMELA

MWENGE  Uhuru umezindua Mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji katika chanzo cha Igombe-Kabangaja, Wilaya ya Ilemela, uliogharimu sh. milioni 585.

Mradi huo uliotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) na kukamilika kwa asilimia 100, uklenga kuongeza ubora na upatikanaji wa majisafi na salama, utawanufaisha wakazi na wananchi 34,000 wa kata za Bugogwa, Shibula, Kahama na Sangabuye.

Akizungumza wakati wa uzinduzi leo , Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Mwang’onda, alisema kuwa  mradi huo  ni muhimu kijamii,  unagusa maisha ya wananchi moja kwa moja, kwa sababu utaongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, na kuchangia kuboresha afya zao na ustawi wa jamii.

Aidha,  baada ya kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita, Wizara ya Maji na MWAUWASA, kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maji inayolenga kutatua kero na changamoto za wananchi na kuboresho huduma za jamii.

“Ahadi ya Mh. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kumtua mama ndoo kichwani, amemtua ndoo kichwani ya majisafi na salama, niwaombe wananchi na wakazi wa Igombe, tuendelee kutunza miradi na miundombinu hii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Mwang’onda.

Msimamizi wa miradi wa MWAUWASA, Mhandisi Nuhu Said, alisema mradi huo umejumuisha ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji, tenki la kuhifadhi maji, pampu mbili za kusukuma maji na ulazaji ya mabomba ya kusafirisha maji.

“MWAUWASA itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha uwekezaji katika miundombinu ya maji unaondelea, unaleta matokeo chanya na kuboresho maisha ya wananchi kijamii, kiafya na kiuchumi,” alisema.

Mhandisi Said alisema kuwa, mradi huo wa upanuzi wa mtambo wa kuchuja maji katka chanzo cha Igombe-Kabangaja,  umetekelezwa kwa ushirikiano kati ya MWAUWASA NA VEI kwa sh. milioni 585, ulianza kutekelezwa Oktoba Mosi, 2024 na kukamilika Jun 30, 2026, ukilenga kuongeza ubora wa maji safi kwa wakazi wa kata nne.

Kwa mujibu wa Msimamizi miradi huyo, mradi huo umejengwa na mkandarasi EQUIPLUS Company , umezalisha ajira 25 kwa vijana, umeleta manufaa kwa kuongeza ubora wa maji kwa kwango cha juu, hivyo utaipatia mamlaka uwezo wa kuandika maandiko miradi ili kupata miradi ya kupanua mtandao wa maji na maunganisho ya wateja.

“Tunamshukuru Rais Dk. Samia, kwa kutuwezesha kutekeleza mradi huu wenye tija na manufaa kwa wakazi na wananchi wa Bugogwa, Kahama, Shibula na Sangabuye na kuaondelea adha ya upungufu wa maj,”alisema Mhandisi Said.