Ofisa Ubora kutoka TIRA Kanda ya Ziwa Halfani Isango akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)
Na Hellen Mtereko,Mwanza
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Nchini (TIRA) iliandaa Kijiji cha Bima katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi kwa kushirikisha kampuni mbalimbali lengo ikiwa ni kutoa elimu kuhusu bima za kilimo,ufugaji na uvuvi.
Hayo yalibainishwa na Ofisa Ubora kutoka TIRA Kanda ya Ziwa, Halfani Isango alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye Kijiji cha Bima katika maonesho hayo yaliyofanyika Nyamhongoro Jijini Mwanza.
Amesema kwenye maonesho hayo Kijiji cha Bima kilipokea wageni zaidi ya 4,000 huku wengine wakiwafikia kupitia vyombo vya habari ambapo aliwasihi wananchi kufika katika ofisi mbalimbali za Bima kwaajili ya kupata elimu na kukata bima itakayolinda shughuli zao.
“Tunawasihi sana wananchi wawe na utaratibu wa kulinda shughuli zao za kilimo,ufugaji na uvuvi kwa kukata bima ambazo zitawasaidia pindi wanapokuwa wamepata majanga”,Amesema Isango
Kwaupande wake Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Kampuni ya Bima ya Reliance, Monica Kijuu alieleza, kampuni hiyo inatoa bima ya kilimo na ufugaji ili kuwawezesha wakulima na wafugaji kufanya shughuli zao kwa amani huku wakijua kuwa wanaweza kufidiwa pale watakapopata majanga.
Amesema majanga yanayoweza kuathiri kilimo ni pamoja na ukame, mvua nyingi, mafuriko pamoja na wadudu.
Naye Meneja wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Kanda ya Ziwa, Stella Marwa alisema,shirika hilo linatoa bima za ajali na maisha ikiwemo bima ya kilimo inayomkinga mkulima dhidi ya ukame, wadudu, mvua nyingi na majanga mengine yanayoweza kusababisha mavuno pungufu.
Marwa amesema NIC pia inatoa elimu kwa wavuvi wanaotumia vizimba na njia za kawaida, ambapo bima inaweza kulinda dhidi ya majanga kama magonjwa na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoweza kuua samaki au vifaranga,endapo mawimbi yataharibu nyavu au keji, mvuvi mwenye bima anaweza kufidiwa na kurejea katika shughuli zake.
Amesema wavuvi wa mitumbwi pia wanapaswa kukata bima kwa ajili ya vyombo vyao na maisha yao, akieleza kuwa injini ya boti ikipata hitilafu mvuvi anaweza kufidiwa. Aidha, mvuvi akipata ajali ziwani na kufariki, familia yake inaweza kupata fidia huku akibainisha kuwa wavuvi wengi bado hawakati bima za vyombo vyao wala bima binafsi.
Hata hivyo amesema,bima pia inaweza kumsaidia mkulima, mfugaji au mvuvi kupata huduma za kifedha ikiwemo mikopo kutoka taasisi za fedha, kwa kuwa bima huongeza ulinzi wa dhamana huku pale hasara inapotokea, fidia humsaidia mhusika kurejesha mtaji na kuendelea na shughuli zake bila kulazimika kutafuta fedha nyingine za kuanzia upya.Meneja wa Kanda ya Ziwa Kampuni ya Bima ya Reliance Monica Kijuu.
Meneja wa Kanda ya Ziwa Kampuni ya Bima ya Reliance Monica Kijuu.
