Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiagana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women), nchini Tanzania, Bi. Julia Broussard, baada ya kumalizika kikao cha Waziri wa Fedha na Ujumbe kutoka Shirika hilo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Waziri, Treasury Square jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiongoza Kikao chake na Ujumbe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women), Ukiongozwa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women), nchini Tanzania, Bi. Julia Broussard, ulipomtembelea Ofisini kwake, Treasury Square jijini Dodoma.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women), nchini Tanzania, Bi. Julia Broussard, akizungumza wakati wa kikao na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), hayupo pichani, alipomtembelea Ofisini kwake, Treasury Square jijini Dodoma.
Kikao cha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), na Ujumbe wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women), nchini Tanzania katika Ukumbi wa Mikutano wa Waziri wa Fedha, Treasury Square jijini Dodoma.

Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje, Bw. Melckzedek Mbise, (wakwanza kushoto), Kamishna Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Bajeti ya Serikali, Bw. Andambike Mololo, (wapili kushoto) pamoja na Wataalamu wengine wa Wizara ya Fedha, wakifuatilia kikao cha Mhe. Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), hayupo pichani, na Ujumbe wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women), nchini Tanzania, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Waziri, Treasury Square jijini Dpodoma.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), (watano kulia), akiwa katika picha ya pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women), nchini Tanzania, Bi. Julia Broussard, (watano kushoto), Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje, Bw. Melckzedek Mbise, (watatu kulia), Kamishna Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Bajeti ya Serikali, Bw. Andambike Mololo (wa kwanza kulia), Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, pamoja na wajumbe kutoka UN Women, baada ya kumalizika kikao cha Mhe. Balozi Omar (Mb) na Ujumbe huo. (Picha na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini, WF – Dodoma)
Na. Josephine Majura na Asia Singano, WF – Dodoma.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya bajeti na usimamizi wa fedha za umma kwa kuzingatia usawa wa kijinsia, hatua inayolenga kuhakikisha rasilimali za Serikali zinatumika kwa ufanisi katika kuchochea maendeleo jumuishi.
Mhe. Balozi Omar (Mb), aliyasema hayo jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women), nchini Tanzania, Bi. Julia Broussard, katika Ukumbi wa Mikutano wa Waziri wa Fedha, Treasury Square jijini Dodoma.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Wizara ya Fedha na UN Women, hususani katika utekelezaji wa Bajeti inayozingatia Masuala ya Kijinsia (Gender-Responsive Budgeting – GRB).
‘’Serikali ya Tanzania, inatambua umuhimu wa kuzingatia masuala ya kijinsia katika sera za fedha, mchakato wa uandaaji wa bajeti, ugawaji wa rasilimali na ufuatiliaji wa utekelezaji wa programu za Serikali ili kuhakikisha mipango ya kitaifa inachangia katika kujenga uchumi jumuishi na wenye usawa’’ alisema Mhe. Balozi Omar (Mb).
Alisema Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027, imezingatia usawa wa jinsia huku Serikali ikiona umuhimu wa kuandaa Taarifa Maalum ya Bajeti inayozingatia Masuala ya Kijinsia (Gender Budget Statement) kama sehemu ya mfumo rasmi wa usimamizi wa fedha za umma.
Alibainisha kuwa hatua hiyo inaweka msingi wa kuimarisha Mfumo wa Uandaaji wa Bajeti Unaozingatia Masuala ya Kijinsia (GRB), utakaosaidia kuhakikisha masuala ya kijinsia yanaingizwa kikamilifu katika mipango, uandaaji wa bajeti, ugawaji wa rasilimali na ufuatiliaji wa utekelezaji wa programu za umma.
“Muhimu siyo tu kuangalia kiasi cha fedha kilichotengwa au kutumika, bali pia matokeo yanayopatikana kutokana na rasilimali hizo na kupima matokeo ya matumizi ya fedha za umma’’. Alisema Mhe. Balozi Omar (Mb).
Aliongeza kuwa, katika kuhakikisha rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake zinafuatiliwa kwa ufanisi, mfumo wa Gender Budget Tagging unaopangwa kuanzishwa utakuwa nyenzo muhimu ya kubaini, kufuatilia na kuchambua matumizi ya bajeti yanayolenga masuala hayo.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN Women), nchini Tanzania, Bi. Julia Broussard alisema Wizara ya Fedha ina nafasi muhimu katika kuhakikisha Tanzania inapata na kutoa taarifa zinazohitajika kuhusu Kiashiria cha 5.c.1 cha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 5), kinachopima uwepo wa mifumo ya kufuatilia na kuweka wazi mgao na matumizi ya rasilimali za umma kwa ajili ya kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.
Alisema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha, katika kuimarisha mifumo na uwezo wa kitaasisi unaohitajika ili kuhakikisha masuala ya kijinsia yanaingizwa kikamilifu katika mipango, bajeti na usimamizi wa rasilimali za umma.
Ushirikiano huo unalenga kuimarisha matumizi ya takwimu na taarifa za bajeti katika kufanya maamuzi, kufuatilia rasilimali zinazotengwa kwa masuala ya kijinsia na hatimaye kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanaongeza matokeo chanya kwa wananchi, hususan katika kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na viongozi Mbalimbali wa Wizara ya Fedha, akiwemo Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje, Bw. Melckzedek Mbise, Kamishna Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Bajeti ya Serikali, Bw. Andambike Mololo pamoja na Wataalamu wengine wa Wizara ya Fedha.
