NA DENIS MLOWE, DAR ES SALAAM
VICTORIA Group (VG) imetangaza kuwa mbio za VG Fun Run zitafanyika kila mwaka tarehe 8 Agosti, huku kamati ya maandalizi ikipendekeza mbio hizo kuongezwa kutoka kilomita 10 hadi nusu marathon ya kilomita 21 kuanzia mwaka 2027.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Victoria Group, Sabasaba Mushingi, wakati akizungumza katika hafla ya kuhitimisha VG Fun Run 2026, iliyoshirikisha wanachama wa kundi hilo, wadau na washirika mbalimbali.
Mushingi alisema uamuzi wa kuifanya VG Fun Run kuwa tukio la kudumu utatoa fursa kwa wanachama kukutana, kubadilishana mawazo na kuendelea kujenga afya zao kupitia mazoezi.
“Kuanzia mwaka huu tutakuwa na VG Fun Run kila tarehe 8 mwezi wa nane permanently, ili tuweze kupata fursa ya kukutana na kubadilishana mawazo na kujenga afya zetu,” alisema.
Alimpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya VG Fun Run, Isidori Msaki, pamoja na timu yake kwa kufanikisha maandalizi ya tukio hilo, akisema kutokana na mafanikio hayo, sekretarieti inaweza kumteua Msaki kuwa mwenyekiti wa kudumu wa kamati ya maandalizi.
Mushingi pia alitoa shukrani kwa wadhamini na washirika wa tukio hilo, akiwataja CRDB Foundation, Victoria Group, Victoria Finance, Victoria Insurance Brokers na wadau wengine kwa mchango wao katika kufanikisha mbio hizo.
Aidha, aliwashukuru Jeshi la Polisi pamoja na timu ya huduma za ambulance kwa kuhakikisha usalama na ustawi wa washiriki wakati wa mbio hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ukopeshaji wa CRDB, Musa Lwila, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa CRDB Foundation, Tully Mwambapa, alisema CRDB ni mmoja wa wadau wakubwa wa VG Group na Victoria Finance, huku akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika afya ya jamii.
Lwila, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CRDB Fitness Club, alisema afya bora ni msingi wa uzalishaji na maendeleo ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla.
“Sisi ni wadau wakubwa wa uwezeshaji katika nchi hii. Hatuwezi kuwa productive bila kuwa na afya zilizo bora. Magonjwa mengi, ikiwemo presha na kisukari, yanahitaji pia tuzingatie afya zetu,” alisema.
Alisema CRDB Foundation itaendelea kuunga mkono juhudi za VG Fun Run, huku akiahidi kuwa katika mbio za mwaka 2027 atashirikisha wanachama wa CRDB Fitness Club ili kuongeza hamasa katika tukio hilo.
“Naahidi mwakani nitawaletea CRDB Fitness Club ili kuja kuwachagiza tukija kama 50 hivi, patapendeza. Sisi tunakuja na vigoma,” alisema.
Lwila pia aliwakaribisha washiriki wa VG Fun Run kwenye tukio la “Sauti Moja” linaloandaliwa na CRDB, akisema benki hiyo imeandaa burudani mbalimbali pamoja na wasanii kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Naye Meneja maendeleo ya biashara Victoria Finance Plc, Dionizi Sabi, alisema Victoria Finance na Victoria Insurance Brokers zitaendelea kuunga mkono juhudi za VG Group katika kuhamasisha afya na ustawi wa jamii.
Sabi alisema afya na uchumi vina uhusiano mkubwa, akiwataka wajasiriamali kutumia fursa zinazotolewa na Victoria Finance kupata huduma za mikopo kwa ajili ya kukuza shughuli zao.
“Afya inaendana na uchumi. Naomba mkaribie Victoria Finance kwa huduma za mikopo ya aina zote,” alisema.
Alisema Victoria Insurance Brokers pia inatoa huduma za bima za aina mbalimbali, hivyo wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kujilinda dhidi ya changamoto zinazoweza kujitokeza katika shughuli zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya VG Fun Run, Isidori Msaki, alisema mafanikio ya mbio hizo yamewapa hamasa ya kuanza maandalizi mapema kwa ajili ya tukio lijalo.
Msaki alisema lengo ni kuhakikisha mwaka 2027 VG Fun Run inafikia kiwango cha nusu marathon ya kilomita 21, huku washiriki wakielekea hadi Mbweni.
“Hii tumeita Fun Run 2026. Mwaka kesho tuanze mazoezi sasa hivi, ili mwaka kesho tuende mpaka Mbweni. Sasa hivi kibali tunataka tuite ni half marathon, kilomita 21,” alisema.
Alisema maandalizi ya mbio hizo yataanza mara baada ya kumalizika kwa tukio la mwaka huu, akisisitiza umuhimu wa washiriki kuendelea kufanya mazoezi ili kujiandaa kwa changamoto kubwa zaidi mwaka ujao.
VG Fun Run 2026 iliwakutanisha wanachama na wadau mbalimbali katika mbio na matembezi yaliyolenga kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi na kuzingatia afya.
Baada ya kukamilika kwa mbio hizo, washiriki walipata nafasi ya kushiriki katika burudani na chakula, huku viongozi wakisisitiza kuwa tukio hilo liendelee kuwa sehemu ya kujenga mshikamano, afya na mahusiano miongoni mwa wanachama wa Victoria Group na wadau wake.