Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo kwa Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI na taasisi za utafiti, akitaka kuimarishwa kwa maonesho ya Nanenane, huduma za ugani, tafiti na utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji.

Akihutubia katika kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Dkt. John Samuel Malecela jijini Dodoma Agosti 8, 2026, Rais Samia ameelekeza kuongezwa kwa kanda za maonesho ya Nanenane pamoja na kuendelea kufanyika kwa ufungaji Maonesho ya Kitaifa jijini Dodoma huku ufunguzi ukifanyika katika kanda zingine.

Aidha, amezielekeza Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani za Kilimo (NAESA) unatekeleza majukumu yake kwa tija na ufanisi.

Amebainisha kuwa shughuli zinazotokana na utekelezaji wa wakala huo zinapaswa kuwa sehemu ya mifumo ya mamlaka za Serikali za Mitaa katika ngazi zote, ili kuimarisha dhana ya ugatuzi wa madaraka na kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi wanaolengwa.

Rais Samia amezielekeza pia taasisi za utafiti wa kilimo, mifugo na uvuvi nchini kuendelea kufanya tafiti za ubunifu pamoja na teknolojia za kisasa na rafiki zitakazoweza kutumiwa na wananchi kuongeza tija na uzalishaji.

Ameongeza kuwa Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI pamoja na wadau wengine wanapaswa kuendelea kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, akibainisha kuwa migogoro hiyo imepungua kiasi lakini bado kuna haja ya kufanya kazi zaidi.

Rais Samia amesema wakulima na wafugaji wote ni muhimu katika uzalishaji, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi na taifa kwa ujumla, hivyo hakuna sababu ya makundi hayo kuendelea kugombana.

Aidha, amewataka washiriki wa Maonesho ya Nanenane kuhakikisha maarifa, teknolojia na uzoefu walioupata katika maonesho hayo havishii kwenye viwanja vya maonesho, bali vitumike kwenye mashamba, maeneo ya uvuvi, baharini, maziwa na katika shughuli za ufugaji.

Pia, amezindua na kukabidhi magari 48 kwa awamu ya kwanza kwa ajili ya Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani za Kilimo (NAESA), yatakayotumika katika utekelezaji wa majukumu ya wakala huo.

Aidha, ametoa wito kwa Wizara, mamlaka, Serikali za Mitaa, taasisi za umma, sekta binafsi na wadau wengine kushirikiana na NAESA ili iweze kutekeleza majukumu yake na kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.