Afisa masoko wa kampuni hiyo ,Veronica Lyimo akizungumza kwenye maonesho hayo ya nanenane Njiro Arusha .
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha .Kampuni ya watengenezaji na wauzaji wa maziwa ya Asili Dairy iliyopo Njiro Arusha imetumia maonesho ya Nanenane kutoa elimu kuhusu umuhimu wa unywaji wa maziwa kwa makundi mbalimbali ya jamii, ikiwemo wanawake wajawazito, wanafunzi na walimu waliotembelea banda la kampuni hiyo.
Afisa Masoko wa kampuni hiyo ,Veronica Lyimo akizungumza kwenye maonesho hayo amesema kuwa, ushiriki wao katika maonesho hayo umekuwa fursa ya kutoa elimu zaidi ya kuuza bidhaa zao.
Amesema kampuni hiyo imekuwa ikitoa elimu mashuleni na katika maeneo mbalimbali ya jamii kuhusu umuhimu wa unywaji wa maziwa, hususani kwa watoto na wanafunzi ambao wako katika hatua muhimu ya ukuaji.
“Hatuuzi maziwa tu, bali tunatoa pia elimu, tunakwenda mashuleni na maeneo mbalimbali ili kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kunywa maziwa,” amesema Lyimo.
Amesema kuwa, maziwa yana virutubisho muhimu kwa wanafunzi, ikiwemo protini na nishati inayowasaidia kupata nguvu na kuendelea vizuri na shughuli zao za kila siku hivyo kampuni imeendelea kutoa elimu kwa wanafunzi na walimu wanaotembelea banda hilo wakati wa maonesho.
Amefafanua kuwa, kampuni hiyo pia imekuwa ikitoa maziwa kwa bei zinazozingatia uwezo wa wananchi wa makundi mbalimbali ya kiuchumi, ambapo bidhaa zao zinapatikana hadi kwa bei ya Shilingi 100 hatua ambayo inamwezesha mtu yoyote kumudu gharama .
Lyimo amewataka wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata maziwa mara kwa mara, na kusisitiza gharama isiwe kikwazo kwa familia zenye kipato cha chini, kwa kuwa kuna bidhaa zinazopatikana kwa bei nafuu.
“Tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua juhudi zetu na ushirikiano wake, ambao umetuwezesha kupata tuzo ya Mshindi wa Pili usindikaji mazao ya kilimo na mifugo.
“Tunawashukuru pia wateja wetu pamoja na wafugaji wetu kwa ushirikiano na kuendelea kutuamini kwani ushindi huu si wa Asili pekee, bali ni ushindi wa wateja wetu kutoka Kaskazini na Kusini, pamoja na wadau wetu wote wanaotuunga mkono.”amesema Lyimo.
“Tunawapenda na kuwathamini sana kwa sababu bila wao tusingefikia hatua hii. Tunamshukuru Mungu kwa kila jambo na kwa kutuwezesha kufikia mafanikio haya.”ameongeza Lyimo.
Aidha amesema kuwa kampuni hiyo inaendelea kuhakikisha inazalisha na kusambaza maziwa yenye ubora kwa wananchi, huku ikifanya kazi kwa kuzingatia taratibu za kiutendaji na usimamizi wa kampuni.
Lyimo amefafanua zaidi kuwa,kampuni hiyo inapata maziwa kutoka kwa wafugaji pamoja na mifugo inayomilikiwa na kampuni, hatua inayosaidia kuhakikisha upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya uzalishaji pamoja na kuwahakikishia wafugaji soko la uhakika.
Amesema maziwa hayo yamekuwa yakifanya vizuri sokoni kutokana na ubora wake na uwezo wa kampuni kuyasambaza kwa wateja katika maeneo mbalimbali.
“Maziwa yetu tunapata kutoka kwa wafugaji, lakini pia tuna ng’ombe wetu. Hivyo tunahakikisha tunapata maziwa yenye ubora wa hali ya juu na katika mazingira masafi na kuyasambaza sokoni,” amesema Lyimo.
Ameongeza kuwa kampuni hiyo imeendelea kupanua upatikanaji wa bidhaa zake, ambapo maziwa yake yanapatikana katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Arusha, Karatu, Manyara na Dar es Salaam.
Lyimo amefafanua kuwa, ushiriki wa kampuni hiyo katika maonesho ya Nanenane umekuwa fursa muhimu ya kuwafikia wananchi, kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa unywaji wa maziwa na kuwawezesha kupata bidhaa hizo kwa urahisi.

