Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C_SDTP) kinara katika hili
Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Stephen Michael, ameeleza kuwa sekta ya maziwa ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia uchumi wa nchi kupitia sekta ya mifugo.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 07,2026 kwenye Banda la Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP) katika maonesho ya 88 yanayoendelea kwenye viwanja vya DKt. John Malecela vilivyopo Nzuguni Dodoma, Amesema tathmini iliyofanyika ilibaini kuwa ifikapo mwaka 2030 kutakuwepo na upatikanaji mdogo wa maziwa endapo hakutakuwa na uwekezaji wa kutosha, kutokana na kuongezeka kwa kipato cha wananchi, ukuaji wa idadi ya watu na kasi ya watu kuhamia mijini.
Aidha, amesema mradi wa C-SDTP wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 231 utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 10, ukiwa na lengo la kuongeza uzalishaji wa maziwa, kuimarisha upatikanaji wa malighafi kwa viwanda na kuiwezesha Tanzania kuwa muuzaji wa maziwa katika masoko ya nje badala ya kuendelea kuwa muagizaji.
Stephen ameongeza kuwa, mradi huo utatekelezwa kwa kutumia mfumo wa ‘corridor approach’ katika maeneo yenye uwezo mkubwa wa uzalishaji wa maziwa, huku ukizingatia mnyororo wa thamani ili kuongeza upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya kusindika maziwa. Ameainisha eneo la mradi ni Pamoja na Mikoa ya Arusha, Iringa, Mbeya, Njombe, Tanga, Morogoro, Pwani na Kilimanjaro kwa Tanzania Bara na Zanzibar ni Mikoa yote mitano ikiwemo Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba.
Amebainisha kuwa mradi utahusisha ushiriki mkubwa wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia upatikanaji wa ng’ombe bora wa maziwa kwa ruzuku, ujenzi wa vituo vya ukusanyaji wa maziwa (Milk Collection Centers na Milk Collection Points) pamoja na kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa maziwa kwenda viwandani.
Amesema, kwa sasa Tanzania bado ni muagizaji wa maziwa, hususan maziwa ya unga, licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa uzalishaji, na kwamba utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji, kuimarisha usindikaji na kuiwezesha Tanzania kuwa muuzaji wa maziwa katika masoko ya nje ndani ya kipindi cha miaka 10.
Kwa upande wake, Mratibu wa Taifa wa Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP), Dkt. Lazaro Kapella, amesema mradi huo umejikita katika maeneo makuu matatu ambayo ni upatikanaji wa ng’ombe bora, upatikanaji wa maji pamoja na kuimarisha afya na udhibiti wa magonjwa ya mifugo, huku ukiunganisha wafugaji na masoko kupitia vituo vya kukusanya maziwa na wanunuzi ili kuimarisha mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Aidha ,amesema Kuwa mradi huo unatarajiwa kunufaisha wafugaji wasiopungua laki saba na kaya laki moja na elfu 40 ndani ya miaka 10, pamoja na kuwezesha upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kupitia ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na taasisi nyingine za fedha kwa ajili ya kununua ng’ombe bora, vifaa vya uchakataji na usafirishaji.
Lengo la mradi wa C-SDTP ni kuongeza uzalishaji, tija na ustahimilivu wa mifumo ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa kutumia teknolojia zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi. Mradi pia unalenga kuboresha upatikanaji wa masoko, kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi na kupunguza athari za mazingira katika tasnia ya maziwa.
Kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa na afua zinazolenga soko, mradi unawawezesha wafugaji wadogo kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa maziwa, kuongeza kipato cha kaya, kuboresha usalama wa chakula na lishe, pamoja na kuendeleza mifumo endelevu ya uzalishaji wa maziwa.
Mradi wa C-SDTP unafadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), OPEC Fund, Green Climate Fund – GCF, na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (Tanzania Agricultural Development Bank – TADB).
