Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Meneja wa Usajili na Leseni wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bi. Mwahija Irika, amesema mbolea hai ni sehemu muhimu ya kuongeza tija shambani na inapaswa kutumika sambamba na mbolea za viwandani ili kuboresha rutuba ya udongo na kuongeza uzalishaji.
Akizungumza katika Ukumbi wa Midahalo wa Wizara ya Kilimo wakati wa mjadala wa kilimo ikolojia uliofanyika Agosti 5, 2026 katika Maonesho ya Nanenane jijini Dodoma, amesema maonesho hayo yameiwezesha TFRA kukutana na wadau mbalimbali, wakiwemo Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM) na wazalishaji wa mbolea hai, kwa lengo la kujadili namna ya kuendeleza sekta hiyo.
Amebainisha kuwa Serikali kupitia Mkakati wa Taifa wa Kilimo Ikolojia Hai wa mwaka 2023–2030 pamoja na bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2026/2027 inaendelea kuhamasisha uzalishaji, usajili na matumizi ya mbolea za asili ili kuongeza upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakulima.
Bi. Mwahija amesema TFRA imeendelea kutoa elimu kwa wazalishaji kuhusu taratibu za usajili wa mbolea hai na kuwahamasisha kusajili bidhaa zao ili ziweze kuingia sokoni rasmi.
Amesisitiza kuwa matumizi ya mbolea hai ni sehemu ya usimamizi bora wa rutuba ya udongo, huku akiwashauri wakulima kupima afya ya udongo kabla ya kutumia mbolea ili kupata matokeo bora ya uzalishaji.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM), Bw. Paul Chilewa, amesema ushirikishwaji wa wadau wa mbolea hai katika banda la TFRA umeongeza uelewa kuhusu usajili wa mbolea na kufungua fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.
Naye mzalishaji wa mbolea ya KEPI, Bw. Elibarti Kimaro, amesema baada ya kukamilisha taratibu za usajili kupitia TFRA, bidhaa yake imepata kibali cha kuuzwa rasmi sokoni, hatua iliyomuwezesha kuwafikia wakulima wengi zaidi.

