Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeanza kutekeleza mradi wa (RISE) kwa kutumia vikundi vya kijamii kufanya matengenezo ya kawaida ya barabara, hatua inayolenga kuboresha miundombinu, kuokoa fedha za Serikali na kuongeza ajira kwa wananchi.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea Nzuguni jijini Dodoma, Mratibu wa CBRM kutoka TARURA Makao Makuu, Mhandisi Richard Missa, amesema mpango huo umebuniwa kupitia Mradi wa Rais unaofadhiliwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia na umeanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 katika mikoa minne ambayo ni Tanga, Pwani, Morogoro na Dodoma.
Amesema katika utekelezaji huo, wilaya zinazoshiriki ni Lushoto, Korogwe na Pangani (Tanga), Rufiji na Mkuranga (Pwani), Mvomero na Kilombero (Morogoro), pamoja na Kongwa (Dodoma), ambapo zaidi ya kilomita 1,500 za barabara zimeanza kufanyiwa matengenezo kupitia vikundi vya kijamii zaidi ya 302.
“Wananchi wanafanya kazi za kufungua mitaro, kusafisha makaravati, kufyeka nyasi na shughuli nyingine za matengenezo ya kawaida ambazo zinazuia uharibifu mkubwa wa barabara hasa kipindi cha mvua. Hii inasaidia barabara kudumu kwa muda mrefu na Serikali kuokoa fedha ambazo zingetumika kufanya matengenezo makubwa,” amesema Mhandisi Missa.
Ameeleza kuwa kutokana na mafanikio yaliyopatikana, TARURA imepanga kupanua mpango huo katika mwaka wa fedha 2026/2027 ili utekelezwe katika halmashauri zote nchini.
Kwa mujibu wa Mhandisi Missa, wananchi wanaotaka kushiriki wanapaswa kusajiliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri husika, kisha kupitia mfumo maalumu ulioboreshwa kwa ushirikiano na PPRA, wanaweza kuingia mikataba moja kwa moja na TARURA kwa ajili ya kufanya kazi za matengenezo ya barabara.
Amesema TARURA pia imeandaa miongozo ya Kiswahili inayowaelekeza wananchi hatua kwa hatua namna ya kutekeleza kazi hizo kwa viwango vinavyotakiwa, jambo linalorahisisha ushiriki wao katika shughuli za maendeleo.
Mhandisi Missa amesema mpango huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo, sambamba na utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma inayotaka taasisi za umma kutenga asilimia 30 ya baadhi ya shughuli za manunuzi kwa makundi maalumu ya wananchi.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, zaidi ya vikundi 1,400 vinatarajiwa kunufaika na mpango huo huku TARURA ikilenga kufanya matengenezo ya zaidi ya kilomita 7,000 za barabara kupitia ushiriki wa wananchi nchini kote.
