Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha Julai 30,2026

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, amesema Kongani Mpya ya Viwanda ya Misugusugu katika Manispaa ya Kibaha itakuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Pwani na Taifa, huku ikitarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 1,000 kwa wananchi.

Kunenge alitoa kauli hiyo Julai 28, 2026, alipofanya ziara ya ukaguzi wa eneo la kongani hiyo lenye ukubwa wa hekta 350, lililotengwa na Manispaa ya Kibaha kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.

Aliipongeza Manispaa ya Kibaha kwa kutenga eneo hilo kwa utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuanzisha maeneo ya kimkakati ya uwekezaji ndani ya siku 100.

Sambamba na hilo, Kunenge alikagua mradi wa maegesho ya magari makubwa ya mizigo katika eneo la Misugusugu, akisema utasaidia kuondoa changamoto ya malori kuegeshwa kandokando ya barabara, kuongeza usalama barabarani na kutoa huduma muhimu kwa viwanda vitakavyoanzishwa katika kongani hiyo.

Aliagiza taasisi zinazowezesha uwekezaji zikiwemo TANROADS, TARURA, TANESCO, DAWASA na TTCL kuhakikisha zinakamilisha miundombinu muhimu kwa wakati ili kuvutia wawekezaji na kuwezesha uzalishaji kuanza mapema.

Kunenge alisema ushirikiano kati ya Serikali, halmashauri na taasisi mbalimbali ni msingi wa mafanikio ya mradi huo, ambao unatarajiwa kuifanya Kibaha kuwa kitovu cha maendeleo ya viwanda katika Mkoa wa Pwani.

Akitoa taarifa ya mradi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, alisema eneo hilo tayari lina huduma za maji na umeme, hivyo kuwa kivutio kwa wawekezaji wa viwanda mbalimbali, ikiwemo vya kutengeneza viatu na nguo za jinsia.

Alisema kongani hiyo inatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 1,000, kuongeza mapato ya Serikali na Halmashauri pamoja na kuimarisha shughuli za uzalishaji na biashara katika Manispaa ya Kibaha.

Kuhusu mradi wa maegesho ya magari makubwa, Dkt. Shemwelekwa alisema ulianza rasmi Julai 1, 2026 na kwa sasa wastani wa magari 90 huingia na kuegeshwa kila siku, hatua iliyopunguza kero ya malori kuegeshwa katika maeneo yasiyo rasmi na kuimarisha utaratibu katika sekta ya usafirishaji