Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akisalimiana na Balozi wa Jamhuri ya Kenya nchini Tanzania, Mhe. Catherine Karemu, alipofika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha rasmi kufuatia kuanza majukumu yake nchini, leo katika Ukumbi wa Ikulu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Kenya nchini Tanzania, Mhe. Catherine Karemu, alipofika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha rasmi kufuatia kuanza majukumu yake nchini. Mazungumzo hayo yalifanyika leo ,katika Ukumbi wa ikulu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akikabidhiwa zawadi na Balozi wa Jamhuri ya Kenya nchini Tanzania, Mhe. Catherine Karemu, alipofika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha rasmi kufuatia kuanza majukumu yake nchini, leo katika Ukumbi wa Ikulu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Kenya nchini Tanzania, Mhe. Catherine Karemu, alipofika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha rasmi kufuatia kuanza majukumu yake nchini, leo katika Ukumbi wa Ikulu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.
……………
ZANZIBAR, 27 JULAI 2026
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar itaendelea kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji na Kenya, akieleza kuwa uhusiano wa kihistoria na kidugu baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kenya umeendelea kuleta manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, Julai 27, 2026, alipokutana Ikulu Zanzibar na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Catherine Karemu, aliyefika kujitambulisha rasmi baada ya kuanza majukumu yake nchini.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuendeleza ushirikiano na Kenya katika sekta mbalimbali, hususan biashara, uwekezaji, utalii, usafiri wa anga na Uchumi wa Buluu.
Amesisitiza umuhimu wa taasisi zinazosimamia viwango katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kushirikiana kwa karibu katika kuratibu viwango vya bidhaa, kuondoa vikwazo vya biashara na kurahisisha upatikanaji wa masoko ya kikanda.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inaendelea na hatua za kukamilisha ujenzi wa Bandari ya Shumba, iliyopo Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambayo itaimarisha usafirishaji wa abiria na bidhaa kati ya Pemba na bandari za Kenya, hususan Mombasa.
Amesema kukamilika kwa bandari hiyo kutachochea biashara, kupunguza gharama za usafirishaji na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi wa Pemba na wafanyabiashara wa pande zote mbili.
Akizungumzia usafiri wa anga, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuimarishwa kwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Zanzibar na Kenya kutachangia kukuza utalii, biashara, uwekezaji na mwingiliano wa wananchi wa mataifa hayo mawili.
Vilevile, ameyakaribisha makampuni binafsi kutoka Kenya kutumia fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar, hususan katika utalii, Uchumi wa Buluu na sekta nyingine za kimkakati zinazochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira.
Kuhusu sekta ya mwani, Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar ni miongoni mwa wazalishaji wakuu wa zao hilo barani Afrika na iko tayari kushirikiana na Kenya katika kubadilishana uzoefu, kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani na kupanua masoko ya bidhaa zinazotokana na mwani.
Kwa upande wake, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Catherine Karemu, ameahidi kutumia muda wake wa kazi kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Kenya na Tanzania, hususan Zanzibar, katika biashara, uwekezaji, utalii, usafiri na sekta nyingine za maendeleo.
Amesema Kenya itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutambua na kuendeleza fursa mpya za ushirikiano zitakazowanufaisha wananchi wa mataifa hayo mawili.