Na John Walter -Babati 
Wakulima wa Mkoa wa Manyara wameendelea kuunga mkono mfumo wa Wakusanyaji Mazao (Aggregators), wakieleza kuwa umewawezesha kuuza mazao yao kwa urahisi, kupata huduma karibu na maeneo yao pamoja na kuondokana na ucheleweshaji wa huduma uliokuwa ukijitokeza kupitia baadhi ya vyama vya ushirika.
Hayo yamebainishwa katika Ripoti ya Utekelezaji wa Shughuli za Wakusanyaji Mazao kwa msimu wa ufuta 2026/2027, ambayo inaonyesha kuwa jumla ya tani 3,416 za ufuta zilikusanywa na kuingizwa kwenye Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kupitia Aggregators 10 waliotekeleza shughuli zao katika Wilaya za Babati Mjini na Babati Vijijini. 
Akizungumza kuhusu ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Wakusanyaji Mazao Mkoa wa Manyara, Philipo Fabiano, amesema Aggregators wanafanya kazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zote zilizowekwa na Serikali, akisisitiza kuwa wao si walanguzi bali ni wakusanyaji mazao wanaotambuliwa rasmi katika mfumo wa biashara ya mazao.
“Sisi tunafanya kazi kwa kufuata taratibu zote zilizowekwa na mamlaka husika. Hatuna shughuli za udalali wala ulanguzi, bali tunakusanya mazao na kuyapeleka kwenye mfumo rasmi wa Stakabadhi za Ghala kwa manufaa ya wakulima na Taifa,”* amesema Fabiano.
Kwa upande wake, Katibu wa Wakusanyaji Mazao Mkoa wa Manyara, Kaji Sijaona, amesema mkulima ana uhuru wa kuchagua kuuza mazao yake kwa Aggregators au kupitia vyama vya ushirika, lakini Aggregators wameendelea kupata imani kutokana na kutoa maamuzi ya haraka na huduma zinazokidhi mahitaji ya wakulima.
“Ni hiari ya mkulima kuchagua anapouza mazao yake. Sisi tupo kutokana na mapungufu yaliyopo kwenye baadhi ya vyama vya ushirika ambapo mara nyingi maamuzi huchukua muda mrefu. Aggregators tunawahudumia wakulima kwa wakati,” amesema Sijaona.
Naye Kaimu Meneja wa Chemba ya wafanyabiashara Mkoa wa Manyara (TNCC), Annamariam Leone Moshi, amesema mfumo wa Aggregators una faida ya kufanya maamuzi kwa haraka tofauti na baadhi ya vyama vya ushirika ambavyo hulazimika kusubiri vikao kabla ya kufanya maamuzi muhimu ya biashara.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa mfumo wa Aggregators umechangia kuongeza ushindani wa soko, kuboresha bei ya mazao, kupunguza gharama za usafirishaji kwa wakulima, kutoa ajira za muda kwa vijana na kuongeza uwazi katika biashara ya mazao kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.