Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Upendo Wella (kushoto), na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania, Bi. Fatma Abdalla (kulia), wakipanda na kumwagilia mti katika Shule ya Msingi Usule, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, ikiwa ni sehemu ya shughuli za uwajibikaji kwa jamii zilizotekelezwa na Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania wakati wa hafla ya uzinduzi wa kituo chake cha 100 cha huduma za mafuta nchini, kilichozinduliwa mkoani Tabora tarehe 22 Julai 2026. Kama sehemu ya uzinduzi huo, Kampuni hiyo pia ilikabidhi madawati 100 kwa Shule ya Msingi Usule kwa lengo la kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati na kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora na salama ya kujifunzia, pamoja na kutoa magodoro 100 kwa Kituo cha Kulelea Watoto cha Istiqaama kwa ajili ya kuboresha mazingira ya maisha ya watoto wanaoishi katika kituo hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Upendo Wella (katikati), akikata utepe kuzindua rasmi kituo cha 100 cha huduma za mafuta ya rejareja cha Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania nchini, kilichopo eneo la Usule, Mkoa wa Tabora. Kituo hicho ni cha kwanza cha Kampuni hiyo mkoani Tabora na kitawawezesha wakazi wa Tabora na maeneo jirani kupata huduma za mafuta, vilainishi vya Puma, gesi ya kupikia ya PumaGas pamoja na fursa za kujipatia pointi kupitia mpango wa Puma Pris. Uzinduzi huo ni sehemu ya upanuzi wa mtandao wa huduma za mafuta wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania unaolenga kuimarisha upatikanaji wa nishati salama na ya uhakika nchini. Hafla hiyo iliyofanyika tarehe 22 Julai 2026 ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Meya wa Manispaa ya Tabora, Mheshimiwa Gulam Dewji (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania, Bi. Fatma Abdalla (wa pili kushoto), Katibu Tawala wa Wilaya ya Tabora, Bi. Asha Churu (wa pili kulia), pamoja na mmiliki wa kituo hicho, Bw. Kishimba Kibera (kulia).
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Upendo Wella (kushoto), akipokea dawati kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania, Bi. Fatma Abdalla (kulia), ikiwa ni sehemu ya madawati 100 yaliyotolewa na Kampuni hiyo kwa Shule ya Msingi Usule, iliyopo Kata ya Mbugani, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora. Msaada huo unaolenga kupunguza changamoto ya upungufu wa madawati na kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora na salama ya kujifunzia ni sehemu ya shughuli za uwajibikaji kwa jamii zilizotekelezwa na Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania wakati wa uzinduzi wa kituo chake cha 100 cha huduma za mafuta nchini, kilichozinduliwa mkoani Tabora tarehe 22 Julai 2026.
………….
Na Mwandishi Wetu
Tabora, Julai 22, 2026 – Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania imezindua rasmi kituo chake cha 100 cha huduma za mafuta nchini, hatua inayodhihirisha kuendelea kwa uwekezaji wake katika sekta ya nishati na kupanua huduma zake hadi mkoani Tabora kwa mara ya kwanza.
Kituo hicho kilizinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, mbele ya viongozi wa serikali, wananchi, wateja pamoja na viongozi wa kampuni hiyo. Kimejengwa katika eneo la kimkakati mjini Tabora ili kuhudumia sekta za biashara, kilimo na usafirishaji, huku kikitarajiwa kuongeza fursa za ajira na kuchochea shughuli za kiuchumi mkoani humo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania, Bi. Fatma Abdalla, amesema kufikiwa kwa vituo 100 ni uthibitisho wa imani ya kampuni katika uchumi wa Tanzania na dhamira yake ya kuendelea kuwekeza kwa manufaa ya wananchi.
“Kufikisha kituo chetu cha 100 cha huduma za mafuta ni zaidi ya kupanua mtandao wetu. Ni ushahidi wa ushirikiano wetu wa muda mrefu na Tanzania na imani ambayo wateja wetu wameendelea kutupatia.
Tunaamini kuwa upatikanaji wa mafuta ya uhakika unafungua fursa na maendeleo,” amesema Bi. Abdalla.
Ameongeza kuwa kila uwekezaji unaofanywa na kampuni hiyo unaimarisha miundombinu inayowezesha biashara, kuunganisha jamii na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa, huku wakiahidi kuendelea kutoa huduma salama na zenye ubora.
Mbali na uzinduzi wa kituo hicho, Puma Tanzania ilitekeleza shughuli mbalimbali za uwajibikaji kwa jamii ikiwemo kutoa magodoro 100 kwa Kituo cha Kulelea Watoto cha Istiqaama, madawati 100 kwa Shule ya Msingi Usule pamoja na kupanda miti 100 kwa kushirikiana na wanafunzi na wananchi wa eneo hilo ili kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, ameipongeza Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania kwa kufikia hatua hiyo muhimu, akisema uwekezaji huo unaonesha imani ya wawekezaji katika uchumi wa Tanzania na utachochea maendeleo ya mkoa huo.
“Uzinduzi wa kituo cha 100 cha Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania ni hatua muhimu inayoonesha imani ambayo wawekezaji wanaendelea kuwa nayo katika uchumi wa Tanzania. Uwekezaji kama huu unaimarisha miundombinu, unaleta ajira, unaunga mkono biashara za ndani na kuchangia maendeleo endelevu ya jamii,” amesema Wella.
Kampuni ya Nishati ya Puma Tanzania imesema itaendelea kupanua mtandao wake wa huduma nchini kwa kuwekeza kwa uwajibikaji, kudumisha viwango vya juu vya usalama na ubora wa huduma pamoja na kujenga thamani ya pamoja kwa wateja, jamii na Taifa.
