Ofisa kazi Mkuu kutoka ofisi ya Waziri Mkuu idara ya kazi Odo Hekela akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miongozo ya ya ukuaji wa uchumi endelevu kwa wazalishaji wadogo Jijini Dodoma leo Julai 20, 2026.

………….

Wazalishaji na wasindikaji wadogo nchini wanatarajiwa kupata urahisi zaidi wa kutekeleza masharti ya uzalishaji baada ya Serikali kuandaa mwongozo utakaowawezesha kujipima kabla ya kufanyiwa ukaguzi na mamlaka mbalimbali.

Mwongozo huo unalenga kuwapa wazalishaji uelewa wa mahitaji yanayohusu mazingira, ajira, afya na usalama kazini pamoja na ubora wa bidhaa, ili waweze kufikia viwango vinavyotakiwa katika soko la ndani na la kimataifa.

Akizungumza katika kikao cha wadau kilichofanyika Jumatatu Julai 20, 2026 jijini Dodoma, Ofisa Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Kazi, Odo Hekela, amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuunganisha taasisi za Serikali zinazohusika na usimamizi wa viwango na kuondoa changamoto ya ukaguzi unaofanywa na taasisi nyingi kwa wakati mmoja.

Amesema lengo si kuzuia shughuli za wazalishaji, bali kuwawezesha kufanya uzalishaji unaokidhi matakwa ya sheria na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania.

“Tunataka mzalishaji ajione kama anavyojiangalia kwenye kioo. Ajue mapema kama ametimiza viwango vinavyotakiwa kabla ya ukaguzi,” amesema Hekela.

Ameeleza kuwa baadhi ya wazalishaji wadogo hukumbana na changamoto kutokana na kutofahamu taratibu zinazohusu mazingira, mikataba ya kazi, mishahara, usalama kazini na masuala ya ajira kwa watoto.Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Kanda wa NEMC Mkoa wa Morogoro, Joyce Omolo, amesema mwongozo huo umesaidia kurahisisha utekelezaji wa sheria za mazingira kwa kuwapa wawekezaji nafasi ya kujihakiki mapema.

Naye Ofisa Mradi kutoka IUCN, Samuel Kajiba, amesema utekelezaji wa dhana ya ukuaji wa uchumi endelevu utasaidia kuunganisha uzalishaji, uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema kupitia mradi wa SUSTAIN, unaoendelea hadi mwaka 2030 katika awamu ya kwanza, juhudi zinaendelea kujenga mifumo endelevu ya uzalishaji wa chakula na kulinda mifumo ya ikolojia.