Zanzibar, Julai 19, 2026 – Meya wa Manispaa ya Mjini, Ibrahim Mohamed (Raza Lee), amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za kuandaa matukio ya burudani yanayowaunganisha wananchi na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi visiwani humo.
Raza Lee alitoa kauli hiyo wakati wa Fanzone Zanzibar iliyoandaliwa na kampuni ya huduma za fedha kidijitali Mixx kwa kushirikiana na Electronics Hub Zanzibar, ambapo maelfu ya wakazi wa Zanzibar walijumuika katika eneo la Kisonge kushuhudia fainali ya Kombe la Dunia 2026 kati ya Spain na Argentina kupitia skrini kubwa zenye ubora wa hali ya juu.
Alisema matukio ya aina hiyo yanaendelea kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha burudani na michezo, huku yakikuza mshikamano wa wananchi na kutoa fursa zaidi za shughuli za kijamii na kiuchumi.
Tukio hilo lililohitimisha mfululizo wa Fanzone Zanzibar lilihudhuriwa na viongozi wa Serikali, wadau mbalimbali na mashabiki wa soka waliopata fursa ya kufuatilia mchezo huo katika mazingira salama, yenye burudani na mshikamano.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa Mixx Zanzibar, Salum Nassor Mohamed, alisema kampuni hiyo itaendelea kuwekeza katika shughuli zinazowaunganisha Watanzania na kuwapatia uzoefu unaokwenda zaidi ya huduma za kifedha.
“Mixx ni zaidi ya pesa. Tunaamini huduma zetu zinapaswa pia kuwaleta watu pamoja kupitia matukio yanayogusa jamii na kuwapa wateja wetu uzoefu wa kipekee,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Electronics Hub Zanzibar, Naif Skandar Ibrahim, alisema ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili umewezesha kwa mara ya kwanza kuandaliwa kwa Fanzone ya kiwango hicho Zanzibar, hatua iliyowapa mashabiki wa soka fursa ya kusherehekea Kombe la Dunia 2026 kwa pamoja.
Alisema tukio hilo limeonyesha jinsi ushirikiano kati ya sekta binafsi unavyoweza kuandaa matukio yenye viwango vya kimataifa yanayochochea burudani, biashara na mshikamano wa jamii.
Baada ya mchezo huo kumalizika, mashabiki waliohudhuria walieleza kufurahishwa na maandalizi ya tukio hilo, wakisema limewapa nafasi ya kushuhudia fainali ya Kombe la Dunia katika mazingira yenye hadhi na burudani ya kipekee bila kulazimika kusafiri nje ya Zanzibar.
Mbali na kufuatilia mchezo huo, waandaaji waliendesha droo ya zawadi mbalimbali kwa washiriki, zikiwemo televisheni, majokofu na zawadi nyingine, hatua iliyoongeza hamasa na kuifanya Fanzone Zanzibar kuwa moja ya matukio makubwa ya kusherehekea fainali ya Kombe la Dunia 2026 visiwani humo.

