Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni (Mb), amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Pwani, wilaya, halmashauri na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuongeza usimamizi wa masuala ya mazingira kwenye viwanda , ili kuepusha hatua ya kuvifungia kutokana na kukiuka sheria za mazingira.
Alitoa agizo hilo alipoweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Kituo cha Biashara cha ATN kilichopo Kata ya Picha ya Ndege, Manispaa ya Kibaha, ikiwa ni mwanzo wa ziara yake mkoani Pwani itakayodumu hadi Julai 23, 2026, ambapo anatarajia kutembelea wilaya za Bagamoyo, Mkuranga na Rufiji.
Masauni alieleza, viwanda vinapaswa kuzingatia sheria za mazingira kwa kuwa kutofanya hivyo kunaweza kusababisha athari kubwa za kiafya na kimazingira, jambo ambalo Serikali haiwezi kulivumilia.
Aidha, aliwaasa wananchi, hususan vijana, kuacha kupotoshwa kupitia matumizi yasiyo na tija ya mitandao ya kijamii na badala yake kuilinda amani na Muungano kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Amani na usalama wa nchi hii ni jambo la kwanza, Muungano ni roho yetu, hivyo vijana wanapaswa kurithishwa utulivu na amani iliyopo,” alisisitiza Masauni.
Vilevile, alieleza Mkoa wa Pwani unaongoza nchini kwa kuwa na viwanda vingi, hivyo aliwataka vijana kukimbilia fursa zinazotokana na uwekezaji huo badala ya kubaki watazamaji.
Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kusimamia agenda ya mazingira kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alieleza sekta ya viwanda imeendelea kuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi wa mkoa huo, huku idadi ya viwanda ikiongezeka kutoka 1,631 hadi 1,722 mwaka 2026.
Alisema viwanda 335 vimejengwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, huku zaidi ya viwanda 80 vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Awali, akiwasilisha taarifa ya mradi wa Kituo cha Biashara cha Picha ya Ndege, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, alisema mradi huo ni wa kimkakati unaotekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani.
Alisema utafiti uliofanywa na halmashauri ulibaini kuwa sehemu kubwa ya mikopo inayotolewa kwa vikundi vya vijana hutumika kulipia maeneo ya kufanyia biashara, hali inayowafanya wanufaika kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati.
“Eneo hili litawawezesha vijana kupata sehemu salama na rasmi ya kufanyia biashara, kukuza mitaji yao na kuendeleza shughuli za kiuchumi,” alielezea Shemwelekwa.
Alibainisha kwamba, mradi huo unagharimu Sh milioni 534.147, huku hadi sasa Sh milioni 292,465,668 zikiwa zimetumika, sawa na asilimia 55 ya utekelezaji.
Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka, alifafanua ,kituo hicho cha biashara kitakuwa mkombozi kwa vijana kwa kuwa kitawawezesha kupata mazingira bora ya biashara na kujijengea uwezo wa kiuchumi.
Aliongeza kuwa Manispaa ya Kibaha inaendelea kujenga vituo vingine vya biashara katika maeneo ya Kwambonde na Misugusugu, huku ikijivunia ongezeko la mapato lililofikia Sh bilioni 26 katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, alisema kwa sasa vituo vitatu vya biashara vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, huku lengo likiwa ni kujenga vituo 10.
Alieleza zaidi ya vijana 150 wanatarajiwa kunufaika na Kituo cha Biashara cha Picha ya Ndege pamoja na maeneo jirani.
Naye kijana Godfrey Maliti aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuvutia wawekezaji nchini na mkoani Pwani, lakini akaomba vijana wazawa wapewe kipaumbele cha ajira katika viwanda vilivyopo.
Katika ziara hiyo, Masauni pia aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule mpya ya mchepuo wa Kiingereza katika Kata ya Kongowe, mradi unaotarajiwa kuboresha upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi wa Manispaa ya Kibaha, Shule hiyo imepokea Sh milioni 404.657 kutoka mapato ya ndani ya manispaa.
Miradi mingine ni mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha kilovoti 132/33 cha Mlandizi, unaolenga kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme na ujenzi wa shule mpya ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika eneo la Mlandizi–Kawawa.

