Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba amesema kuwa hesabu za awali za mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2026 zinaonesha kuwa thamani ya Mfuko imefikia zaidi ya shilingi trilioni 11.6, thamani ambayo imeendelea kuwa chachu katika uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuongeza thamani ya fedha za wanachama.

Bw. Mshomba ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habarı Julai 17, 2026 jijini Dar es Salaam kuhusu msamaha wa tozo kwa waajiri wenye malimbikizo ya michango na tozo itokanayo na ucheleweshaji wa michango.

Ameeleza kuwa ukuaji huo umetokana na ongezeko la michango ya wanachama, uwekezaji wenye tija, maboresho ya mifumo ya utoaji huduma pamoja na matumizi ya teknolojia katika kuongeza ufanisi wa shughuli za Mfuko na kusisitiza kuwa Mfuko huo utaendelea kushirikiana kwa karibu na waajiri, wafanyakazi na wadau wote kuhakikisha mfumo wa hifadhi ya jamii nchini unaendelea kuwa jumuishi, endelevu na wenye kuleta manufaa kwa Watanzania wote.

“Katika kuhakikisha fedha za wanachama zinaendelea kuzaa thamani na kuchangia maendeleo ya Taifa, NSSF imeendelea kutekeleza uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuongeza thamani ya fedha za wanachama, kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuunga mkono maendeleo ya sekta mbalimbali za uzalishaji ambapo uwekezaji wa Mfuko umejikita katika maeneo mbalimbali ikiwemo hati fungani, dhamana za Serikali, hisa, miradi ya kimkakati, milki na amana za benki”, amesema Bw. Mshomba.

Ameongeza kuwa, mafanikio hayo yanatoa wajibu mkubwa zaidi wa kuendelea kusimamia rasilimali za wanachama kwa uadilifu na kuhakikisha mfumo wa hifadhi ya jamii nchini unaendelea kuwa imara, endelevu na wenye manufaa kwa Watanzania wote.

Mkurugenzi Mshomba ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi, chenye thamani ya takribani shilingi bilioni 354 ambacho kinamilikiwa kwa ubia kati ya NSSF yenye asilimia 96 na Jeshi la Magereza kupitia Shirika lake la Uzalishaji Mali lenye asilimia 4 ambapo hadi kufikia Machi 2026, jumla ya tani 45,594 za sukari zimezalishwa na ajira 11,315 zikiwemo ajira 2,315 za moja kwa moja na ajira 9,000 zisizo za moja kwa moja zimezalishwa.

Vile vile, NSSF imeanza kupanua wigo wa uwekezaji nje ya Tanzania baada ya kupata kibali kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), uwekezaji unaolenga masoko ya mitaji na miradi ya majengo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ikiwemo ujenzi wa majengo ya biashara jijini Nairobi, Kenya hatua inayolenga kuongeza mapato ya uwekezaji, kupunguza vihatarishi vya uwekezaji na kuimarisha uwezo wa Mfuko wa kutimiza wajibu wake kwa wanachama.