Dar es Salaam
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amemtaka Mkandarasi China Road and Bridge Corporation (CRBC) kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara chini ya Mradi wa Uboreshaji Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II), akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia ucheleweshaji unaoweza kuwanyima wananchi huduma kwa wakati.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya miradi hiyo katika wilaya za Ubungo na Kinondoni, Mhandisi Seff amesema bado hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji katika baadhi ya maeneo na kumtaka mkandarasi huyo kuongeza nguvu kazi, vifaa na usimamizi ili kuhakikisha miradi yote inakamilika ndani ya muda uliokubaliwa kwenye mikataba
“Mmeomba kuongezewa muda ili mkamilishe kazi, hivyo ni lazima muongeze nguvu na kasi ya utekelezaji ili kufidia muda uliopotea na kukamilisha kazi kulingana na tarehe za mikataba, kinyume na hapo tutalazimika kuvunja mkataba na kuwapa watu wenye uzoefu zaidi ili kulinda maslahi ya serikali na wananchi”, amesisitiza Mhandisi Seff.
Aidha, amemtaka mkandarasi huyo kuzingatia usimamizi wa ubora na usalama kazini kwa kuweka alama za usalama barabarani ili kuwaelekeza wananchi na kuepusha ajali maeneo ya ujenzi.
Hata hivyo, Mtendaji Mkuu huyo amepongeza kukamilika kwa madaraja makubwa ya Msumi na Goba–Wakorea ambayo yalikuwa kero kubwa kwa wananchi na tishio la kiusalama hasa wakati wa msimu wa mvua.
”Kukamilika kwa madaraja haya ni faraja kubwa kwa wananchi. Ndiyo maana tumekuwa tukisisitiza makandarasi kuanza utekelezaji kwenye maeneo yenye shida zaidi ili kuleta ahueni ya haraka”, amesema.
Mhandisi Seff amewashukuru wananchi kwa kuendelea kutoa taarifa pale wanapoona kazi hazifanyiki kwa ufasaha na pia kwa kutoa mrejesho pale miradi inapotekelezwa vizuri akitolea mfano mradi wa Daraja la Msumi.
Mwisho amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa mkandarasi na wasimamizi wa mradi hususan katika kipindi hiki cha kusubiri malipo ya fidia zao kwa baadhi ya maeneo kwa kupisha maeneo hayo ili ujenzi uendelee bila kukwama.
Katika ziara hiyo Mhandisi Seff ametembelea na kukagua miradi katika Wilaya ya Ubungo ambayo ni ujenzi wa daraja la Msumi na barabara ya Msumi (Km 9.9), barabara ya Goba-Wakorea (Km 7.76) Hondogo Shija (Km 4.16), Sheikh Bofu (Km 1.13), Juma Ikangaa (Km 0.97), Posta Matembe (Km 0.82), Segesera (Km 0.82), Ubungo NHC (Km 0.45), Msikitini (Km 0.37) pamoja na Sinza KKKT (Km 0.27) ambazo zote ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Katika wilaya ya Kinondoni amekagua ujenzi wa barabara ya Nakalekwa–Bwawani (Km 7.32), Umoja (Km 3.86), Mahakamani (Km 0.693), Mivumoni (Km 4.79), Tegeta–Silverz (Km 2.00), Shoko-Mongela (Km 3.04), Msikitini Bima (Km 0.77), Bima–Viwandani (Km 1.25), Makoka (4.04 KM), Shauri Madai (Km 3.37), Makonde (Km 1.89) Kanisa (Km 1.09), Mivumoni (Km 4.79) na kupokea taarifa ya utekelezaji wa barabara nyingine za mitaani zinazoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na zege.

