Maadhimisho ya 5 ya Siku ya Kiswahili Duniani yamefikia kilele jijini Bujumbura, Burundi, huku viongozi wa Afrika Mashariki wakitoa wito wa kuongeza jitihada za kukuza na kuimarisha matumizi ya Kiswahili kama nyenzo ya kuleta umoja, mshikamano na maendeleo.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo, mgeni rasmi ambae ni Waziri wa Vijana michezo na Utamaduni wa Jamhuri ya Burundi Bi. Lyidia Nsekela amesema Kiswahili kimeendelea kuwa daraja muhimu la mawasiliano na utangamano wa wananchi wa Afrika Mashariki na Bara la Afrika kwa ujumla. Ameeleza kuwa ni wajibu wa nchi wanachama kuwekeza zaidi katika ufundishaji, matumizi na uendelezaji wa lugha hiyo ili kizazi kijacho kiweze kunufaika na urithi huo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Mhe. Hamis Mwijuma, amewasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameipongeza Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) kwa juhudi za kuendeleza ajenda ya Kiswahili katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mhe. Mwijuma amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama katika kukuza Kiswahili kama lugha ya kimataifa ya mawasiliano, elimu na diplomasia, akisisitiza kuwa lugha hiyo ni urithi wa pamoja na nyenzo muhimu ya kuimarisha amani, mshikamano na maendeleo.
Naye Katibu Mtendaji wa KAKAMA, Dkt. Caroline Asiimwe, amesema maadhimisho hayo ni fursa ya kutafakari safari ya Kiswahili, mafanikio yaliyopatikana na kupanga mustakabali wake katika dunia inayobadilika kwa kasi. Ameishukuru Serikali ya Burundi kwa maandalizi na ushirikiano uliowezesha kufanyika kwa kongamano na maadhimisho hayo.
Ameongeza kuwa maendeleo ya Kiswahili yanahitaji ushirikiano wa pamoja wa serikali, taasisi za elimu, vyombo vya habari na wadau mbalimbali ili kuhakikisha lugha hiyo inaendelea kutumika katika maeneo ya elimu, teknolojia, biashara na diplomasia.
Siku ya Kiswahili Duniani huadhimishwa kila mwaka Julai 7 tangu ilipotangazwa na UNESCO mwaka 2021, hatua iliyokifanya Kiswahili kuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa kwa siku maalumu ya kimataifa ya kuadhimishwa duniani.
