NA DENIS MLOWE IRINGA 

MBUNGE wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo huku akiahidi kufuatilia kwa karibu changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na wakazi wa Kijiji cha Mlandege, Kata ya Mseke.

 

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi, Kiswaga aliwashukuru wakazi wa Kalenga kwa kumchagua tena kuwa mbunge na kueleza kuwa baada ya kukamilika kwa kikao cha Bajeti ya Serikali bungeni, sasa ni wakati wa kurejea kwa wananchi ili kusikiliza maoni na changamoto zao kwa lengo la kuziwasilisha serikalini.

 

Alisema Jimbo la Kalenga limeendelea kuwa mfano wa utulivu na amani wakati wa uchaguzi, hali ambayo imechangia maendeleo na ukuaji wa uchumi, huku akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa.

 

Kiswaga alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, maji, umeme na miundombinu, akieleza kuwa fedha za utekelezaji wa bajeti zinatarajiwa kuanza kupelekwa katika halmashauri ili kutekeleza miradi iliyopangwa.

 

Akizungumzia huduma ya umeme, alisema kati ya vitongoji 455 vya Jimbo la Kalenga, vitongoji 331 tayari vimefikiwa na huduma hiyo huku vilivyosalia vikitarajiwa kuunganishwa ifikapo mwaka 2030 au hata kabla ya muda huo.

 

Katika sekta ya kilimo, Kiswaga alisema Serikali inaendelea kutafuta njia za kuhakikisha ruzuku ya mbolea inaendelea kutolewa licha ya changamoto za kibajeti, huku akieleza kuwa wabunge wameendelea kuishauri Serikali kutafuta vyanzo vipya vya fedha ili kuwasaidia wakulima ambao ndio tegemeo la uchumi wa wananchi wengi.

 

Pia aliwahamasisha wananchi kujiunga na mfumo wa bima ya afya kwa wote, akisema mfumo huo utasaidia kupunguza gharama kubwa za matibabu ambazo zimekuwa zikiongezeka kila mwaka na kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi.

 

Kuhusu changamoto ya kushuka kwa bei ya mazao, Kiswaga alisema Serikali inaendelea kutafuta masoko ya ndani na nje pamoja na kuishauri kuongeza uwezo wa kununua mazao kupitia akiba ya taifa ili kuwasaidia wakulima kupata bei nzuri zaidi.

 

Awali, Diwani wa Kata ya Mseke, Alex Kadinda, alimshukuru mbunge huyo kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa katika kutatua changamoto za wananchi.

 

Kadinda alisema moja ya mafanikio yaliyopatikana ni upatikanaji wa mabati 55 aliyotoa Mbunge Kiswaga papo hapo yatakayokamilisha ujenzi wa darasa katika kijiji hicho baada ya awali kuonekana mabati 40 yasingetosha.

 

Aidha aliwasilisha changamoto nyingine zinazohitaji ufumbuzi ikiwemo upatikanaji wa umeme katika Kitongoji cha Genza Ulore, ujenzi wa kalavati ili kurahisisha mawasiliano, kuanzishwa kwa stendi ya mabasi Mlandege pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji.

 

Katika mkutano huo wananchi walieleza kero mbalimbali zikiwemo ukosefu wa zahanati, changamoto za huduma za afya na matumizi ya bima, gharama za michango mashuleni pamoja na kushuka kwa bei ya mazao ya kilimo.

 

Akijibu hoja hizo, Kiswaga aliwataka wananchi kuanza kutenga eneo na kuanzisha ujenzi wa zahanati kwa nguvu zao, akieleza kuwa Serikali hutoa fedha za kukamilisha majengo baada ya hatua za awali za ujenzi kukamilika.

 

Pia aliahidi kufuatilia suala la kuanzishwa kwa stendi ya Mlandege kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto nyingine zilizowasilishwa na wananchi, akisisitiza kuwa ataendelea kuwa sauti yao bungeni ili kuhakikisha huduma za maendeleo zinaimarika katika Jimbo la Kalenga.