Na John Bukuku, Dar es Salaam
Waandishi, watangazaji na waandaji wa vipindi vya watoto wametakiwa kuzingatia maadili na kanuni za kitaaluma katika kuripoti masuala ya watoto ili kulinda usalama, haki na ustawi wao.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha mada katika mafunzo ya siku mbili kwa waandaji na watangazaji wa vipindi vya watoto kuhusu malezi yaliyofanyika katika Ukumbi wa Afed jijini Dar es Salaam na kuhitimishwa leo Juni 18, 2026, Mtaalamu wa Mawasiliano na Utetezi wa UNICEF Tanzania, Usia Nkhoma Ledama, alisema vyombo vya habari vina jukumu kubwa zaidi ya kutoa taarifa kwani vinapaswa pia kutetea maslahi ya watoto na kuhakikisha sauti zao zinasikika kwa manufaa ya maendeleo yao.
“Jukumu la vyombo vya habari katika kuripoti masuala ya watoto si kutoa taarifa pekee, bali pia kutetea maslahi yao, kuimarisha sauti zao na kuhakikisha kuwa simulizi zao zinaleta mabadiliko yenye manufaa katika jamii,” alisema Ledama.
Alisisitiza kuwa kuripoti habari zinazowahusu watoto na vijana hakupaswi kamwe kuwaweka katika hatari, akieleza kuwa waandishi wanapaswa kuheshimu utu na haki za kila mtoto pamoja na kulinda faragha na usiri wa taarifa zao.
Ledama alisema wakati wa kuwahoji watoto, waandishi wanapaswa kuzingatia haki yao ya kusikilizwa, kushiriki katika maamuzi yanayowahusu na kulindwa dhidi ya madhara au vitendo vya kulipiziwa kisasi vinavyoweza kutokea baada ya taarifa kuchapishwa au kurushwa hewani.
“Maslahi bora ya mtoto lazima yawekwe mbele ya jambo lolote lingine, ikiwemo kampeni za utetezi wa haki za watoto. Aidha, maoni ya mtoto yanapaswa kupewa uzito unaostahili kulingana na umri na kiwango chake cha ukomavu,” alisema.
Aliongeza kuwa waandishi wanapaswa kuepuka maswali au maoni yanayoweza kumdhalilisha mtoto, kumweka katika hatari au kumrudishia maumivu ya matukio ya kiwewe aliyoyapitia, huku wakiepuka ubaguzi wa aina yoyote katika kuwachagua watoto wa kuwahoji.
Ledama pia aliwataka wanahabari kuhakikisha kuwa watoto na walezi wao wanafahamu madhumuni ya mahojiano kabla ya kufanyika na kutoa ridhaa ya kushiriki katika mahojiano, kurekodiwa au kupigwa picha.
Kuhusu utambulisho wa watoto, alisema ni muhimu kwa vyombo vya habari kuficha majina na sura za watoto wanaohusika katika matukio nyeti kama vile unyanyasaji wa kingono, maambukizi ya VVU na UKIMWI au wale wanaokabiliwa na mashauri ya jinai ili kuwalinda dhidi ya unyanyapaa na madhara ya muda mrefu.
“Usichapishe habari au picha inayoweza kumweka mtoto, ndugu zake au marafiki zake katika hatari, hata kama utambulisho wao umebadilishwa au kufichwa,” alisisitiza.
Aidha, alisema katika mazingira yenye hatari ya madhara au kulipiziwa kisasi, waandishi wanapaswa kuwa waangalifu zaidi wanaporipoti habari zinazowahusu wakimbizi, watafuta hifadhi au watoto waliowahi kuhusika katika migogoro ya kivita.
Ledama alihitimisha kwa kuwataka wanahabari kuthibitisha usahihi wa taarifa wanazopokea kutoka kwa watoto na, pale wanapokuwa na shaka kuhusu usalama wa mtoto, kuzingatia kuripoti hali ya jumla inayowakabili watoto badala ya kuangazia mtoto mmoja mmoja.
Mafunzo hayo yaliwakutanisha waandaji na watangazaji wa vipindi vya watoto kutoka vyombo mbalimbali vya habari kwa lengo la kuimarisha uelewa kuhusu malezi, ulinzi wa mtoto na maadili ya kitaaluma katika kuripoti masuala yanayowahusu watoto.

