Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amewasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo Jumatano tarehe 20 Mei, 2026 , ambapo Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 2,564,441,414,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akiwasilisha makadirio hayo leo Jumatano Mei 20, 2026 mbele ya Bunge la Tanzania jijini Dodoma, Waziri Ulega amesema bajeti hiyo inalenga kuimarisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu nchini, hususan sekta ya barabara.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo ya bajeti, kati ya Shilingi 2,564,441,414,000 zilizoombwa, Shilingi 97,104,935,000 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida ya Wizara na taasisi zake, huku Shilingi 2,467,336,479,000 zikiwa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Aidha, kati ya fedha za matumizi ya kawaida, Shilingi 92,209,218,000 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, na Shilingi 4,895,717,000 zikiwa ni kwa ajili ya matumizi mengineyo ya uendeshaji wa shughuli za kila siku.

Kwa upande wa bajeti ya maendeleo, fedha za ndani zimepangwa kuwa Shilingi 1,544,872,147,000, wakati fedha za nje ni Shilingi 922,464,332,000. Fedha za ndani zinajumuisha Shilingi 1,047,405,500,000 kutoka Mfuko wa Barabara na Shilingi 497,466,647,000 kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali.

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imeeleza kuwa fedha hizo zitatumika katika ujenzi, ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya barabara nchini ili kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi.