MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hatua yake ya kihistoria ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti, akisema mradi huo ni ukombozi mkubwa kwa sekta ya utalii na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Akizungumza leo Mei 19, 2026 katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Kanali Mtambi amesema uamuzi huo ni matokeo ya maono ya muda mrefu ya wadau wa utalii, viongozi wa serikali pamoja na wananchi wa Mkoa wa Mara waliokuwa wakisisitiza umuhimu wa kuboreshwa kwa miundombinu ya usafiri katika eneo la Serengeti.
Amefafanua kuwa kwa sasa uwanja mdogo uliopo Serengeti ni miongoni mwa viwanja vinavyotumika kwa wingi zaidi nchini, ambapo kwa baadhi ya siku hupokea takribani ndege mia moja mchana pekee, hali inayoonesha wazi uhitaji mkubwa wa uwanja wa kisasa wa kimataifa utakaoendana na hadhi ya eneo hilo.
“Serengeti ni hazina ya kipekee duniani, ni Urithi wa Dunia uliosajiliwa na UNESCO, na ni miongoni mwa maeneo yanayovutia watalii kutoka kila pembe ya dunia kutokana na maajabu ya uhamaji wa wanyama pori na mandhari yake ya kipekee,” amesema Mtambi.
Ameongeza kuwa licha ya umaarufu huo wa kimataifa, bado kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa usafiri wa moja kwa moja, ambapo baadhi ya wageni hulazimika kupitia nchi jirani kabla ya kufika Tanzania, jambo ambalo amesema limekuwa likipunguza kasi ya ukuaji wa sekta ya utalii.
Amesema ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti utabadilisha kabisa taswira ya upatikanaji wa huduma za utalii, kwa kurahisisha safari za moja kwa moja, kuongeza idadi ya wageni, na kufungua fursa kubwa za uwekezaji katika Mkoa wa Mara na maeneo jirani.
Kanali Mtambi pia amebainisha kuwa Mkoa wa Mara una hazina kubwa ya vivutio vya kiutalii, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ziwa Victoria, chemchemi za maji moto (hot springs), pamoja na urithi mkubwa wa kiutamaduni unaojumuisha utofauti wa makabila mbalimbali, jambo linaloufanya mkoa huo kuwa kitovu muhimu cha utalii wa kipekee nchini.
Amesema mkoa huo una zaidi ya makabila mengi yenye utajiri wa mila na tamaduni, hali inayoongeza thamani ya utalii wa kiutamaduni na kuufanya Mkoa wa Mara kuwa na nafasi ya kipekee katika ramani ya utalii barani Afrika.
Aidha, amesisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya barabara, anga na huduma nyingine za kijamii ni msingi muhimu wa kufungua kikamilifu fursa za kiuchumi zilizopo katika mkoa huo, ambazo bado hazijatumika ipasavyo.
Katika hatua nyingine, Kanali Mtambi amesisitiza kuwa Mkoa wa Mara ni salama na unaendelea kuwa miongoni mwa mikoa yenye utulivu mkubwa nchini, akibainisha kuwa mazingira hayo mazuri ni kichocheo muhimu cha uwekezaji na maendeleo ya sekta mbalimbali.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha amani na mshikamano wa kijamii, hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza imani ya wawekezaji na wageni wanaotembelea maeneo ya utalii.
Ameipongeza Serikali na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maamuzi ya kimkakati yanayoendelea kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa utalii barani Afrika, huku akisisitiza kuwa mradi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti utakuwa kichocheo kikubwa cha mageuzi ya kiuchumi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

