Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Bw. Eliakim Maswi, amewataka  watumishi wa Wizara hiyo  kuwajibika ipasavyo na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuongeza utendaji kazi ndani ya Wizara.

Aidha, amebainisha kuwa jambo analolipa kipaumbele ni uwajibikaji kwa watumishi wote, huku akisisitiza kuwa kila mtumishi anatakiwa kutathmini mchango wake katika maendeleo ya Wizara hiyo.Ameyabainisha hayo Mei 18, 2026 wakati wa mapokezi yake katika Ofisi za Wizara hiyo, Mtumba jijini Dodoma. Mapokezi hayo yaliongozwa na Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Dorothy Gwajima, Naibu Waziri Mhandisi Maryprisca Mahundi, Manaibu Katibu Wakuu Wakili Amon Mpanju na Bi. Felister Mdemu pamoja na viongozi na watumishi mbalimbali wa Wizara hiyo.Pia ameongeza kuwa Wizara hiyo ni moja ya Wizara bora, lakini changamoto kubwa ipo kwa watumishi wenyewe kushindwa kubadilisha mtazamo na kuongeza ufanisi wa kazi.

Aidha, amebainisha kuwa hatavumilia uzembe, uongo na tabia ya kupeleka majungu kwa viongozi, akisisitiza kuwa anataka kuona utendaji wa watumishi kwa vitendo badala ya maneno.

Pia ameongeza kuwa watumishi wanapaswa kufika kazini kwa wakati na kufanya kazi kwa bidii, kwani Serikali imewaamini kwa kuwapatia nafasi hizo huku wananchi wengi wakihitaji ajira.Aidha, amesema kuwa watumishi wote wanapaswa kuilinda na kuitumikia Serikali kwa uadilifu, akieleza kuwa matatizo mengi ndani ya taasisi husababishwa na watendaji wenyewe kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Pia, amebainisha kuwa atafanya vikao na idara mbalimbali ili kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi, huku akiwaagiza watumishi kuandika changamoto zao pamoja na sababu zinazowafanya washindwe kutekeleza majukumu yao ipasavyo.