Waswahili husema _Iso kongwe haivuki na Utu uzima dawa_, misemo hii imedhihirika mwishoni mwa wiki hii wakati Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na timu yake walipomualika Waziri mstaafu wa Maliasili na Utalii Mhe. Zakia Hamdan Meghji katika uwasilishaji wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2026/2027 Bungeni Dodoma.
Picha hii inaonesha mkongwe huyo akiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri Mhe. Hamad Chande, Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi na naibu Katibu Mkuu Nkoba Mabula.
Mama Meghji anaheshimika na wizara ya Maliasili na Utalii kutokana na kuhudumu katika wizara hiyo kwa kipindi wa miaka tisa (09) iliyosaidia kuchangia mageuzi na mabadiliko chanya yaliyoimarisha sekta ya utalii, uhifadhi endelevu wa wanyamapori, misitu na malikale za Tanzania. Kutokana na utumishi wake uliotukuka katika wizara hii, amewahi kutunukiwa nishani maalum na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Huyo ndiye Zakia Hamdan Meghji katika enzi zake akijulikana pia kama “Iron Lady” wa
Tanzania, mwanamke pekee aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha kuanzia mwaka 2006 hadi 2008, na kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo nyeti ambapo alifanya kazi kubwa kuimarisha utulivu wa uchumi, kupunguza umaskini na kusimamia uwajibikaji wa serikali kwenye masuala ya fedha.
