Na MWANDISHI, WETU

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutaka Chama kijifanyie tathmini, unalenga kupata viongozi bora na kushughulikia kikamilifu changamoto za Watanzania.

Amesema wakati wana CCM wakielekea katika uchaguzi mkuu wa Chama, ni vyema kila mmoja kujitathmini kabla ya kuomba nafasi ya uongozi kuhakikisha ana sifa zikiwemo za kimaadili.

Wasira aliyasema hayo jana mkoani Kigoma alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM kwa Nyakati tofauti katika wilayani Buhigwe, Kasulu pamoja na Wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Mkoa,  akiwa katika ziara ya kichama mkoani humo.

Alisisitiza viongozi na wanachama wa CCM kuijua na kuizingatia Katiba ya Chama, kanuni na miongozo inayoongoza uendeshaji wa Chama.

“Siku hizi tunasema kuna njia kuu na mchepuko, njia kuu ya chama hiki imeandikwa katika hivi vitabu (Katiba, kanuni na miongozo) mchepuko ni tabia tunayoendesha nayo ambayo inapingana na vitabu, kwa hiyo tumechepuka tunataka kurudi njia kuu. Chama kinachoundwa na katiba hii kina madhumuni,malengo,Sifa za mwanachama, masharti ya kiongozi, wanachama, katiba na Kanuni.

“sifa za uongozi, hizi zipo katika kitabu kinaitwa kanuni za uchaguzi ndani ya CCM, inasema sifa ya kwanza kiongozi wa Chama akinai maadili ya Chama kwa maana ya kwamba ayajue na ayaishi na asiwe mtu wa kuyumbayumba katika mambo ya msingi.

“Unajua unaweza ukachagua kiongozi leo ana hili kesho ana lile sasa unaweza kumuuliza wewe hasa unasimamia nini maana yale uliyoyakubali jana ndiyo unayoyapinga kesho…wewe nawe ni mwanachama hatari na mwanachama wa namna ile anaweza akakidhulumu chama chenyewe.

Makamu Mwenyekiti Wasira alisisitiza kiongozi anapaswa kuwa na uwezo wa kazi anayoiomba.

“Kama wewe unataka kuwa mwenyekiti wa kata na hii inatuhusu baadhi kwa sababu mwaka kesho tuna uchaguzi, uombe kazi unayoiweza, uombe kazi na nafasi ya uongozi unayoiweza kwa wakati huo na usije ukasema unaziweza kwa wakati wote, hapana.

“Tunataka viongozi wa chama hiki kwanza wawe wanachama kwa sababu viongozi wanatokana na wanachama, wanachama wanaoelewa watachagua viongozi wanaoelewa, wanachama ambao hawaelewi watarubuniwa na kumchagua ambaye haelewi kuliko wao, maana uongozi sio utajiri,” alisema.

Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti Wasira, Halmashauri Kuu ya Taifa ilikutana jijini Dodoma hivi karibuni na kuazimia Chama kufanya tathmini ili kujiboresha.

“Halmashauri Kuu ya Taifa imekutana juzi juizi Dodoma, tumekubaliana kwamba tujitathmini, tukitathmini chama chetu na tathmini isitoke juu, itoke kwa wanachama kwenye matawi yao, kwenye kata zao mtuambie hiki chama kama tumekosea, tumekosea wapi tusahihishe nini ili tuweze kusonga mbele.

“Haya si mambo yangu, ni uamuzi wa halmashauri kuu ya taifa tusahihishe, tujisahihishe tujitathmini maana sisi ni Chama cha wanadamu tunaweza kufanya makosa, lakini makosa ni makosa yanaweza yakasahihishwa. Hata ukiwa muumini wa dini yako ukaanguka unaweza ukarudi wakakubatiza upya, huko ni kujisahihisha,” alieleza.

Katika hatua nyingine, Wasira aliwasihi wananchi kutohadaika wala kuvisikiliza vyama vinavyotumika kutaka kurudisha ukoloni.

Alisema vipo baadhi ya vyama vya siasa ambavyo kwa matukio vinaonekana kubeba ajenda za watu walioko nje ya Tanzania kwa maslahi yao.

“Kimekuja Chama hapa kinawaambia sisi tunataka kuchukua nchi, lakini chama hiki kinatumwa na wazungu, wazungu wako nyuma, wazungu wale wanajua ukoloni kurudi kabisa na bunduki ni ngumu, lakini wakikamata viongozi wenu au vibaraka waliowaweka wao wanaweza kuendesha nchi hizi wakanyonya rasilimali za taifa,” alisema.

== ==


MAELEZO PICHA
 
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, akizungumza na viongozi wa CCM  katika wilayani ya Kasulu, akiwa katika ziara ya kuimarisha uhai wa Chama na Jumuiya zake Mkoani Kigoma. ( Picha na Fahadi Siraji)
 
Wanachama na Viongozi wa ccm wilaya ya Kasulu wakitoa Maori tao wakati wa Mkutano wa Makamu Mwenyekiti wa Chama Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira , wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.
shangwe la wanachama na Viongozi katika Mkutano huo