Na Mwandishi Wetu, BRUSSELS
KAMPUNI ya ndege ya Brussels Airlines ya nchini Ubelgiji imeandika historia mpya kwa kutangaza kuanza kwa safari za moja kwa moja kati ya Brussels nchini Belgium na Kilimanjaro International Airport kuanzia Juni 3, 2026.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, safari hizo zitafanyika mara mbili kwa wiki, kila Jumatano na Jumamosi, hatua inayotajwa kuwa chachu mpya kwa sekta ya usafiri wa anga, biashara na utalii nchini Tanzania.
Uzinduzi wa safari hizi unaonekana kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Ubelgiji huku ukirahisisha usafiri kwa watalii, wafanyabiashara na wananchi wa pande zote mbili.
Kuanzishwa kwa safari hizi za moja kwa moja kunatarajiwa kuongeza ushindani wa huduma za usafiri wa anga kwa kupunguza muda wa safari na kutoa chaguo zaidi kwa abiria wanaosafiri kati ya Afrika Mashariki na Ulaya.
Aidha, hatua hiyo inatajwa kuwa muhimu katika kukuza biashara ya kimataifa, hasa kwa bidhaa zinazohitaji usafirishaji wa haraka kama matunda, mboga mboga, maua, minofu ya samaki pamoja na bidhaa nyingine zinazouzwa katika masoko ya Ubelgiji na nchi jirani za Ulaya.
Ubelgiji imeendelea kuwa miongoni mwa washirika muhimu wa Tanzania katika biashara ya bidhaa za kilimo na madini, huku ikiwa moja ya nchi chache za Ulaya ambapo thamani ya bidhaa zinazotoka Tanzania kwenda nchini humo ni kubwa kuliko bidhaa zinazoagizwa kutoka huko.
Katika sekta ya utalii, safari hizi mpya zinatarajiwa kuongeza idadi ya watalii kutoka Ubelgiji na mataifa jirani ya Ulaya wanaotembelea vivutio maarufu vya Tanzania kama Serengeti National Park, Ngorongoro Conservation Area na Mount Kilimanjaro.
Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watalii kutoka Ubelgiji imeongezeka kwa kasi kutoka takribani watalii 9,000 mwaka 2018 hadi zaidi ya 18,000 mwaka 2024, jambo linalodhihirisha kuimarika kwa mahusiano ya watu wa nchi hizo mbili pamoja na kuongezeka kwa hamasa ya kutembelea Tanzania.
Mafanikio haya yanaelezwa kuwa matokeo ya mahusiano ya muda mrefu na ya kirafiki kati ya Tanzania na Ubelgiji yaliyoendelea kuimarishwa chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia diplomasia ya uchumi, maboresho ya sera, uwekezaji katika miundombinu pamoja na mazingira ya amani na utulivu nchini.
Serikali imewataka wafanyabiashara na wadau wa sekta ya utalii kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na safari hizi mpya ili kuongeza na kukuza biashara, uwekezaji na mapato yatokanayo na utalii pamoja na kuimarisha zaidi uhusiano wa Tanzania na mataifa ya Ulaya.

