
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Botswana, Mheshimiwa Festus Gontebanye Mogae.
Rais Dkt. Samia amemtaja Hayati Mogae kuwa kiongozi aliyetoa mchango muhimu katika uongozi wa Botswana na Afrika kwa ujumla, hususan katika kuimarisha utawala bora, kusimamia uchumi na kuongoza jitihada za kukabiliana na changamoto za afya ya jamii.
Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Dkt. Samia anatoa salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Botswana, Mheshimiwa Duma Gideon Boko, familia ya Marehemu, Serikali na wananchi wa Botswana.
Amesema Tanzania inaungana na Botswana katika kipindi hiki cha majonzi, na inaendelea kuthamini uhusiano wa kindugu na ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Aidha, Rais Dkt. Samia anaiombea familia ya Hayati Mogae, Serikali na wananchi wa Botswana faraja na nguvu katika kipindi hiki cha majonzi, na kumuomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya Marehemu mahali pema peponi.
Bakari S. Machumu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu
