Na. Zainab Ally -Mikumi.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb)amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya utalii nchini ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii Afrika. Alisema uwekezaji unaoendelea katika barabara, kiwanja cha ndege Kikoboga na huduma za malazi utaongeza mvuto wa vivutio vya utalii na kuwafanya watalii kukaa muda mrefu zaidi hifadhini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa hoteli ya kisasa ya “Mikumi Wildlife Lodge” leo mei 08, 2026 ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi, Dkt. Nchemba alisema; “Kiwango cha huduma na ubora wa hoteli hii kitaongeza zaidi hadhi ya Hifadhi ya Taifa Mikumi na kuifanya kuwa moja ya maeneo yanayovutia watalii na wawekezaji wengi zaidi hifadhini”.

Vile vile, Dkt. Nchemba aliongeza kuwa sekta binafsi ina mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya uhifadhi na utalii kwani zaidi ya asilimia 70 ya sekta hiyo inategemea uwekezaji wa watu binafsi.

Kutokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuvinadi vivutio vya utalii kupitia Filamu ya Tanzania; “*The Royal Tour*” umeongeza chachu ya ongezeko la watalii Nyanda za Juu Kusini hasa ikiziunganisha Hifadhi za Taifa Mikumi, Nyerere, Udzungwa pamoja na eneo maarufu kwa utalii wa fukwe – Zanzibar.

“Muunganiko huu utaongeza muda wa watalii kukaa hifadhini muda mrefu, ajira, uwekezaji, mapato kwa serikali na kukuza biashara za wajasiriamali;” aliongeza Dkt. Nchemba.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima alisema kuwa mkoa wa Morogoro unashuhudia ukuaji mkubwa wa sekta ya utalii kutokana na maboresho ya miundombinu ikiwemo reli ya kisasa ya SGR, Uwanja wa Ndege wa Mikumi wa Kikoboga pamoja na uwekezaji wa hoteli hii ya kisasa. 

Aidha, aliongeza; “Kila mwisho wa wiki takribani watalii 5,000 wanaingia mkoani Morogoro wakitokea Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar kuja kutalii Hifadhi ya Taifa Mikumi, hali inayoongeza fursa za kibiashara na ajira kwa wananchi, ukizingatia Morogoro ina sehemu nyingi na nzuri kwa ajili ya malazi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alisema kuwa sekta ya utalii inachangia asilimia 17 ya pato la Taifa huku ikitoa ajira za kudumu na zile za muda mfupi zaidi ya milioni 2.7 kwa Watanzania. Pia aliongeza, idadi ya watalii imeongezeka na kufikia zaidi ya milioni 5.9 kutokana na juhudi za Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji na kutangaza vivutio vya utalii kimataifa.

Hata hivyo Dkt. Kijaji alisema; “Ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi kuna maeneo 11 yaliyotengwa kwa uwekezaji ambapo sita tayari yamechukuliwa huku maeneo matano yakiendelea kusubiri wawekezaji wapya, niwaarike na wengine kuchangamkia fursa hiyo.”

Akisoma risala kwa mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Mikumi Wildlife Lodge Bw. Gulam Ismail alisema; “Hotel hii inamilikiwa na watanzania wazawa kwa asilimia 100 huku tukimiliki miradi mingine 24 inayoendelea na ujenzi, lengo likiwa ni kuwekeza kwenye maeneo yenye vivutio vya utalii ili kuchangia ongezeko la watalii nchini”.

Bw. Gulam aliongeza kuwa wawekezaji wa ndani wanalo jukumu la kuhakiksha sehemu ya faida yao inabaki nchini ili itumike kulijenga Taifa. Hivyo wawekezaji wa ndani wapewe kipaumbele cha kupewa maeneo ya uwekezaji ili kukuza mitaji yao itakayowezesha kutoa ushindani wa kibiashara dhidi ya wawekezaji wa nje.