Tanga
Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Mhandisi Juma Hamsini amesema utekelezaji wa mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) katika Jiji la Tanga ni fursa adhimu ya kulibadilisha jiji hilo kiuchumi na kijamii, hatua inayofanyika kupitia uboreshaji wa miundombinu ya barabara, masoko na maeneo ya fukwe.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Mhandisi Hamsini amesema awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa barabara za lami Kilomita 4.4, ujenzi wa mfereji mkuu unaojumuisha kata ya Maweni na kata zinazoguswa na mafuriko pamoja na jengo la usimamizi wa mradi.
Ameongeza kuwa awamu ya pili inajumuisha ujenzi wa soko la Makorora kata ya Makorora, soko la Samaki (Deep sea) kata ya Chumbageni pamoja na uboreshaji wa fukwe eneo la Raskazone kata ya Central ambapo miradi yote hiyo ina thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 33.
”Miradi hii ikikamilika italeta manufaa makubwa, wananchi watafanya biashara hadi usiku kupitia taa za barabarani, thamani ya nyumba itapanda, ajira zitaongezeka, muonekano wa Jiji utabadilika, mifereji itaondoa mafuriko, shughuli za usafiri na usafirishaji zitaboreka na pia kupitia masoko mapato ya Halmashauri yataongezeka”, amesema.
Naye, Mratibu wa mradi wa TACTIC Jiji la Tanga, Mhandisi Jumaa Jumanne ameeleza kuwa mradi huo unaogharamiwa na mkopo nafuu toka Benki ya Dunia utajenga barabara ya Tangasisi 2 yenye urefu wa Km 2.7, barabara ya Magomeni yenye urefu wa Km 1.7, ujenzi wa mfereji wa Kange-Mwarongo wenye urefu wa Km 10 pamoja na uwekaji wa taa 600 za barabarani.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA wilaya ya Tanga, Mhandisi Boniface Mwambene amesema kupitia mradi huo wataongeza mtandao wa barabara za lami kutoka Km 101 hadi kufikia zaidi ya Km 105 za lami ambapo ujenzi wa barabara hizo utakuwa mkombozi kwa wananchi wa kata za Tangasisi, Masiwani, Duga, Mwanzange na Mbugani.
Naye, Bi. Miriam Kiwambo, Mwenyekiti wa mtaa wa Raskazone, ameishukuru serikali kwa mradi wa kujengewa fukwe kwani utatoa ajira kwa vijana, utaongeza thamani kwani watapata wageni wengi na biashara zitaongezeka.
Bw. Bael Wadhir, Mwenyekiti Chama cha Wavuvi mkoa wa Tanga ameishukuru serikali kwa mradi wa ujenzi wa soko la samaki la Deepsea ambapo amesema mradi huo ukikamilika watafanya biashara bila changamoto.
Naye, mfanyabiashara soko la Makorora, Bw. Musa Karata ameeleza kuwa walikuwa wakifanya biashara kwenye mazingira magumu, soko lao lilikuwa maficho ya wahalifu, mvua ikinyesha kulikuwa na matope, hivyo wanashukuru kujengewa soko jipya wateja wataongezeka na watafanya biashara zao vizuri.

