Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf F. Mkenda, amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya amali nchini kwa lengo la kuongeza fursa za vijana kupata ujuzi na kujiunga na soko la ajira.

Amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, jumla ya wanafunzi 315,307 wamedahiliwa katika vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, idadi ambayo imezidi lengo la wanafunzi 265,000, sawa na asilimia 119 ya utekelezaji. Aidha amebainisha kuwa ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa idadi ya vyuo vya ufundi kutoka 1,414 hadi 1,446 nchini.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo Mei 7,2026 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ameongeza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo 64 vya VETA vya wilaya pamoja na chuo kimoja cha Mkoa wa Songwe, ambapo ujenzi huo umefikia wastani wa asilimia 68, hatua inayolenga kusogeza huduma za mafunzo ya ufundi karibu zaidi na wananchi.

Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara imeendelea pia kuboresha miundombinu ya mafunzo ikiwemo ujenzi wa maabara za TEHAMA katika shule na vyuo vya ufundi ili kuongeza ubora wa ufundishaji na ujifunzaji.

Aidha amebainisha kuwa Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaohitajika sokoni kupitia mafunzo ya vitendo, ili kuwawezesha kujiajiri na kuajiriwa katika sekta mbalimbali za uchumi.

Pia ameongeza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha elimu ya amali nchini na kuhakikisha vijana wanakuwa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya uchumi wa viwanda.