Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika kufundishia na kujifunzia ili kuongeza ubora wa elimu nchini.

‎Amesema kuwa Serikali imeboresha majukwaa ya kidijiti kwa wanafunzi wa sekondari pamoja na kuunganisha mifumo hiyo na teknolojia ya akili unde ili kusaidia wanafunzi kujisomea, kufanya majaribio na kujipima kwa njia ya mtandao. 

‎Akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Elimu kwa Mwaka 2026/2027 Mei 7,2026, Waziri Wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda‎, amebainisha kuwa maabara za TEHAMA zimejengwa katika shule mbalimbali huku vifaa vya kisasa vya kompyuta vikisambazwa ili kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa ya teknolojia tangu wakiwa mashuleni.

‎Pia ameongeza kuwa Serikali itaendelea kubadilisha vitabu vya kawaida kuwa maudhui ya kielektroniki yanayojumuisha video, sauti na majaribio pepe ili kuendana na maendeleo ya teknolojia duniani.