Na OWM – TAMISEMI, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amekemea tabia ya ubaguzi wa wanafunzi wenye mahitaji maalum unaofanywa na baadhi ya shule wakati wa mitihani ya darasa la nne, la saba, kidato cha pili, cha nne na cha sita kwa sababu ya kuhofia kushusha ufaulu wa shule husika, na kuwataka Wakuu wa Mikoa kushughulikia changamoto hiyo.
Prof. Shemdoe amekemea ubaguzi huo Mei 06, 2026 akiwa katika Mkutano wa wadau wa elimu wa Mkoa wa Dodoma uliofanyika katika Ukumbi Wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
“Nitasimamia utatuzi wa changamoto hii ya kubaguliwa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum nchi nzima ili wapate haki ya kufanya mitihani kama wanafunzi wengine,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amewataka walimu katika shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum kuhakikisha wanawaandaa vizuri wanafunzi hao kabla ya mitihani ili waweze kufanya mitihani yao kwa ufanisi.
Prof. Shemdoe amewata viongozi wa elimu wa ngazi zote nchini kuhakikisha wanakuza ubunifu na kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya elimu, huku akitumia fursa hiyo kuupongeza mkoa wa Dodoma kwa kupata ufaulu mzuri katika mtihani wa darasa la saba mwaka 2025.
Aidha, Prof. Shemdoe amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujenga miundombinu bora ya shule za msingi na sekondari ambayo imekuwa ni chachu ya kuongeza ufaulu wa wanafunzi nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kujenga miundombinu bora ikiwepo ya TEHAMA inayomuwezesha mtoto wa kijijini kusoma katika mazingira bora kama ya mtoto wa mjini.

