Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali itaendelea kuongeza fursa kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kuratibu udahili wa wanafunzi 180,000 wanaotarajiwa kujiunga na programu mbalimbali za shahada ya kwanza katika vyuo vya elimu ya juu.
Amesema kuwa itaongeza idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kutoka wanafunzi 252,773 mwaka 2025/26 hadi 292,981 mwaka 2026/27.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo Mei 7,2026 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda,Amebainisha kuwa serikali itaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Stashahada 24,978 katika fani za sayansi na ufundi ambapo hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa elimu ya juu kwa vijana wengi zaidi nchini.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa ufadhili kwa wanafunzi wenye ufaulu wa juu katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati kupitia SAMIA Skolashipu kutoka wanafunzi 2,630 mwaka 2025/26 hadi wanafunzi 2,738 mwaka 2026/27.
Amesema kuwa pia kupitia programu ya Samia Extended Scholarship DS/AI+ itaongeza idadi ya wanafunzi kutoka 50 hadi 100 kwa ajili ya kujiunga na shahada ya kwanza katika vyuo bora vilivyo nje ya nchi katika fani za sayansi data, sayansi shirikishi na akili-unde.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwezesha ufadhili wa masomo katika eneo la sayansi na teknolojia ya nyuklia kwa wanafunzi wa shahada ya umahiri.
