Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf F. Mkenda (Mb.) amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika mafunzo ya walimu wa masomo ya amali ili kuimarisha ubora wa ufundishaji katika vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Amesema kuwa walimu 150 wa masomo ya amali za kihandisi wamepatiwa mafunzo maalum nchini New Delhi, India kwa muda wa mwezi mmoja, ambapo walijengewa ujuzi wa kisasa wa ufundishaji na mbinu shirikishi za kufundisha masomo ya ufundi.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo Mei 7,2026 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amebainisha kuwa walimu hao pia walipata fursa ya mafunzo kwa vitendo katika shule na vyuo vya ufundi nchini humo, hatua inayolenga kuwajengea uwezo wa kufundisha kwa ufanisi zaidi wanaporejea nchini.
Pia ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha rasilimaliwatu katika sekta ya elimu ya ufundi kwa kuhakikisha walimu wanakuwa na ujuzi unaoendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira.
Amesema kuwa uwekezaji huo katika walimu ni msingi muhimu wa kuandaa vijana wenye ujuzi, wenye uwezo wa kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
