Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma
Serikali imeweka wazi mpango wa utekelezaji wa mfumo wa elimu ya lazima ya miaka kumi ambao unalenga kuboresha upatikanaji wa elimu na kuimarisha ujuzi kwa wanafunzi nchini, hatua inayotarajiwa kuanza kutekelezwa rasmi Januari 2028.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Adolf Mkenda amesema kuwa mpango huo utaanza kwa kupokea kwa pamoja wanafunzi wa darasa la sita na saba, ikiwa ni sehemu ya maboresho makubwa ya mfumo wa elimu nchini yanayolenga kuongeza ufanisi na usawa katika upatikanaji wa elimu, akisema kuwa
“kupokea wanafunzi wa darasa la sita na la saba kwa wakati mmoja mwezi Januari 2028.”
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo Mei 7,2026 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ameeleza kuwa utekelezaji wa elimu hiyo ya lazima ya miaka kumi utafanyika kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Elimu, ambapo Serikali itaandaa miongozo, kujenga miundombinu mipya ya shule, na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia pamoja na mafunzo kwa walimu.
Aidha, Serikali imeeleza kuwa maboresho hayo yataambatana na mapitio ya sheria mbalimbali za elimu ili kuziweka taasisi zote muhimu katika mfumo unaoendana na mabadiliko ya kisera na mahitaji ya sasa ya kitaifa na kimataifa.
Katika mpango huo pia, Serikali imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya amali ili kuongeza idadi ya vijana wenye ujuzi wa vitendo, hatua itakayosaidia kupunguza changamoto ya ajira na kuongeza fursa za kujiajiri.
Vilevile, Serikali imeweka mkazo katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu pamoja na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kuhakikisha wahitimu wa mfumo huo mpya wa miaka kumi wanakuwa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
