Na Mwandishi Wetu,Mbinga

MKOA wa Ruvuma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, umejipanga kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa kutoka tani 26,088.05 za msimu 2025/2026 hadi kufikia tani 29,000 katika msimu wa kilimo 2026/2027.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, kwenye hotuba yake iliyosomwa na mkuu wa wilaya ya Mbinga Kisare Makori wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa kahawa kanda ya Ruvuma uliofanyika katika ukumbi wa kanisa katoliki jimbo la Mbinga.

Alisema, kwa sasa wastani wa uzalishaji wa kahawa katika mkoa huo ni tani 26,088,47 ya kahawa kavu huku uzalishaji kwa wakulima wengi ni robo hadi nusu kilo kwa kila mti mmoja kiasi ambacho ni kidogo ikilinganisha na uwepo wa ardhi kubwa yenye rutuba inayofaa kwa kilimo cha zao hilo.

Abbas alisema,lengo la Serikali ya mkoa wa Ruvuma kuhakikisha uzalishaji wa kahawa unaongezeka ili kuendana na malengo ya Taifa kwa kutumia fursa za maeneo makubwa yaliyopo kufanya upanuzi wa mashamba,upatikanaji wa pembejeo za ruzuku na miche bora ambapo katika msimu 2026/2027 Serikali kupitia bodi ya kahawa na wadau wengine imetoa miche 5,770,550 kwa wakulima.

Abbas,amewataka wakulima wa kahawa mkoani humo kuachana na kilimo cha mazoea na badala yake wazingatie kilimo cha kisasa chenye tija ili kuongeza uzalishaji na ubora wa kahawa.

Alisema,Serikali ya chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuotesha miche bora iliyotolewa bure kwa wakulima,ili kuhakikisha zao hilo linakuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wan chi yetu na kupunguza umaskini kwa wananchi hususani wakulima.

“ufufuaji na ukarabati wa mashamba yaliyozeeka na kuimarisha mfumo wa masoko ni miongoni mwa jitihada hizo,kwa mfano msimu 2025/2026 mkulima amelipwa wastani wa Sh.12,000 baada ya makato yote ikilinganishwa na Sh.9,000 msimu uliopita”alisema Abbas.

Alisema,bei katika msimu 2025/2026 ilikuwa nzuri, lakini bado jitihada zinahitajika ili kuboresha bei hizo kwani tatizo la bei isiyoridhisha anayopata mkulima inatokana na ubora hafifu wa kahawa inayoandaliwa,uadilifu wa viongozi wa Amcos na wanunuzi na uuzaji husiofuata taratibu zilizowekwa na mamlaka(magoma).

Amewataka maafisa ugani,kuwajibika zaidi kwa wakulima ili kutoa elimu juu ya kilimo bora na cha kisasa cha zao la kahawa na wadau wengine kuhakikisha kahawa inayozalishwa inakuwa na ubora kwa kuwa ushirikiano kati ya wataalam,wadau na wakulima ndiyo suluhisho la upatikanaji wa kahawa bora.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa uzalishaji na maendeleo ya zao la kahawa kutoka bodi ya kahawa Tanzania Kajiru Kisenge,amewataka wakulima na vyama vya msingi vya ushirika kufanya maandalizi ya msimu mpya wa ununuzi kwa kuhakikisha mizani zitakazotumika kwenye ununuzi wa kahawa zinakaguliwa,wanaandaa mashine za kuchakata kahawa ili kupata kahawa bora.

Alisema,wastani wa uzalishaji wa kahawa hapa nchini ni tani 80,000 huku mkoa wa Ruvuma unazalisha tani 29,000 hivyo mkoa wa Ruvuma kupitia wilaya ya Mbinga una nafasi kubwa katika uzalishaji wa zao la kahawa nchini.

“katika kikao hiki tumekubaliana kuwa na mikakati ambayo itawezesha kuongeza uzalishaji wa kahawa kutokana na bei kuongezeka ili mkoa wa Ruvuma uwe mfano katika uzalishaji wa zao la kahawa hapa nchini na kufikia tani 50,000 kwa mwaka”alisema Kisenge.

Mrajisi msaidizi wa ushirika mkoa wa Ruvuma Venance Msafiri,amewapongeza wakulima na viongozi wa vyama vyamsingi vya ushirika kwa kazi nzuri iliyowezesha mkoa wa Ruvuma kushika nafasi ya pili kwa uzalishaji wa kahawa hapa nchini.

Alisema,Serikali ya mkoa kwa kushirikiana na Amcos,Chama kikuu cha ushirika Mbinga(Mbifacu na bodi ya kahawa Tanzania imejipanga kuongeza uzalishaji wa zao hilo muhimu la biashara ili liweze kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Alisema,Serikali kupitia wizara ya kilimo inaendelea kutafuta ufumbuzi wa baadhi ya changamoto zinazorudisha nyuma sekta ya kahawa ikiwemo kuondoa kero zilizopo na kuhakikisha mkulima anapata bei nzuri.

Msafiri,ameipongeza Mbifacu kuanza matumizi ya mizani za kijiditali katika ununuzi wa kahawa ambazo zimesaidia kupunguza vitendo vya wizi na dhuluma dhidi ya wakulima wa zao hilo.