📌Ashiriki Kongamano la Sekta ya Madini na Nishati nchini Msumbiji*

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema Afrika inahitaji kuimarisha ushirikiano wa kimkakati ili kuhakikisha rasilimali zilizopo zinachangia kikamilifu maendeleo ya uchumi, ukuaji wa viwanda na ustawi wa wananchi wake.

Mhandisi Mramba amesema hayo wakati akichangia mjadala wa ngazi ya juu katika Kongamano na Maonesho ya 12 ya Sekta ya Madini na Nishati ya Msumbiji (MMEC 2026) yanayoendelea jijini Maputo, nchini Msumbiji,

 Kongamano hilo.limehusisha viongozi wa Serikali, wawekezaji na wadau wa sekta ya nishati na madini kutoka mataifa mbalimbali ili kujadili mustakabali wa maendeleo ya rasilimali za Afrika.

Mhandisi Mramba ameeleza kuwa licha ya Afrika kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali za madini na nishati, mchango wa bara hilo katika maendeleo ya viwanda duniani bado ni mdogo, hali inayolazimu nchi za Afrika kuweka mikakati ya pamoja ya kuongeza thamani ya rasilimali hizo badala ya kuendelea kuuza malighafi.

Akitoa mfano wa Tanzania, Mhandisi Mramba amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika uzalishaji wa umeme, matumizi ya gesi asilia pamoja na ujenzi wa miundombinu ya nishati, hatua ambazo zimeongeza upatikanaji wa umeme na kuchochea ukuaji wa uchumi na shughuli za viwanda.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda kupitia miradi ya pamoja ya miundombinu ikiwemo njia za usafirishaji na mitandao ya umeme inayounganisha nchi mbalimbali barani Afrika, akitanabaisha kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Afrika katika soko la kimataifa.

Vilevile amesisitiza kuhusu nchi za Afrika kuwekeza zaidi katika maendeleo ya viwanda, kuimarisha minyororo ya thamani ya kikanda pamoja na kuendeleza ujuzi wa wataalamu ili bara hilo liweze kunufaika zaidi na rasilimali zake.