Serikali imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha utumishi wa umma kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia, uwajibikaji na ufanisi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akifungua Mkutano wa Pili wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala na Rasilimaliwatu (AAPAM) Tawi la Tanzania, unaofanyika jijini Arusha Mei 5–7, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete, alisema mageuzi ya utumishi wa umma yanategemea kwa kiasi kikubwa wataalamu wa utawala na rasilimaliwatu.
Alisema wataalamu hao wana jukumu muhimu la kuhakikisha taasisi za umma zinakuwa na watumishi wenye uwezo, maadili na uzalendo, huku wakisimamia matumizi sahihi ya teknolojia katika utoaji wa huduma.
“Mageuzi ya utumishi wa umma siyo tu kubadili mifumo ya kiteknolojia, bali pia kubadili fikra, mitazamo na utamaduni wa utendaji kazi,” alisema.
Katika hotuba yake, Waziri Kikwete alisisitiza umuhimu wa kujenga uwezo wa kidijitali kwa watumishi wa umma, kuvutia na kuendeleza vipaji hasa kwa vijana, pamoja na kuhakikisha mifumo ya teknolojia inaendana na maadili na uwajibikaji.
Aidha, aliwataka wataalamu hao kusimamia kikamilifu sera, sheria na taratibu zilizopo, pamoja na kuhakikisha haki na usawa vinazingatiwa katika usimamizi wa watumishi.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo alieleza kuridhishwa na utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa mwaka 2025, ikiwemo kuhuishwa kwa Muundo wa Maendeleo ya Utumishi wa kada hiyo na kuwekwa katika daraja la TGS E badala ya TGS D, hatua iliyoboreshwa kuanzia Septemba 2025.
Pia alibainisha kuwa Serikali inaendelea na mchakato wa kuanzisha Bodi ya kitaaluma ya Maafisa Rasilimaliwatu na Utawala, itakayolinda taaluma hiyo pamoja na kusimamia maadili yake.
Kwa upande wa mifumo ya kidijitali, Waziri Kikwete alielekeza matumizi ya mifumo ya kielektroniki ikiwemo e-Uhamisho na e-Utendaji, huku akisisitiza kuachana na matumizi ya barua za kawaida katika michakato ya kiutumishi.
Aliongeza kuwa tathmini za utendaji kazi wa watumishi zinapaswa kufanyika kwa wakati, kwani zinahusiana moja kwa moja na maamuzi ya kiutawala kama upandishaji vyeo na nyongeza za mishahara.
Awali, akizungumzia kaulimbiu ya mkutano huo inayohusu kufikiria upya utoaji wa huduma za umma kwa kutumia teknolojia, Waziri huyo alisema ni muhimu kwa wataalamu hao kuwa chachu ya mabadiliko katika taasisi zao.
Alisisitiza kuwa matokeo ya mkutano huo yanapaswa kutoa mwelekeo wa kimkakati utakaoimarisha utendaji wa utumishi wa umma na kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi.
Mkutano huo uliwakutanisha wataalamu wa utawala na rasilimaliwatu kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili namna bora ya kuboresha utumishi wa umma barani Afrika.

