Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Maji imeendelea kuimarisha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama vijijini, ambapo hadi mwezi Desemba 2025 kiwango cha huduma hiyo kimefikia asilimia 85.2 kutoka asilimia 83.1 mwaka 2024.
Akizungumza bungeni wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso amesema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wa vijijini.
Amebainisha kuwa katika kipindi hicho Serikali imefanikiwa kukamilisha miradi 54 ya maji yenye vituo 946 vya kuchotea maji vilivyonufaisha wananchi zaidi ya 493,932 katika vijiji 151 nchini.
“Kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kumetokana na kukamilika kwa utekelezaji wa miradi hiyo ambayo imeboresha hali ya huduma ya maji vijijini,” alisema Aweso.
Aidha, Waziri Aweso alisema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mingine 992 ya maji vijijini ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha asilimia 90 ya wananchi wa vijijini wanapata huduma ya maji ifikapo mwaka 2030 sambamba na kuimarisha huduma za usafi wa mazingira.
Katika hatua nyingine, Serikali imeendelea kuimarisha usafi wa mazingira vijijini kupitia Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira na Elimu kwa Umma, ambapo matumizi ya vyoo bora kwenye kaya yamefikia asilimia 98.9.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa imechangia kuboresha afya za wananchi pamoja na kupunguza magonjwa yanayotokana na mazingira yasiyo salama.
