NA FAUZIA MUSSA
Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Muhammad Ibrahim Sanya, amefungua kikao cha wadau kilicholenga kukusanya maoni na mapendekezo kuhusu moduli iliyoboreshwa ya uondoaji wa mali za umma kupitia Mfumo wa ZGAMIS.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Kikwajuni, kiliwakutanisha wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali za umma, wakijadili kwa kina namna bora ya kuimarisha mifumo ya usimamizi wa mali za Serikali kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Akifungua kikao hicho, Sanya alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wadau katika hatua hii ya maboresho, akibainisha kuwa maoni yao ni msingi muhimu katika kuhakikisha mfumo huo unakuwa na ufanisi, uwazi na unakidhi mahitaji halisi ya watumiaji wake.
“Ushiriki wenu ni nguzo muhimu katika kufanikisha maboresho haya. Tunahitaji maoni yenu ya kina ili kujenga mfumo imara unaorahisisha usimamizi wa mali za umma kwa tija zaidi,” alieleza.
Katika uwasilishaji wake, Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari, Mawasiliano na Uhusiano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Simai Silima Juma, alifafanua maboresho yaliyofanyika kwenye moduli hiyo, akieleza kuwa yamelenga kuongeza ufanisi, kurahisisha matumizi ya mfumo, pamoja na kuimarisha uwazi katika mchakato mzima wa uondoaji wa mali za Serikali.
Aliongeza kuwa mfumo huo sasa una uwezo wa kuwezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati halisi (real-time), hatua itakayosaidia kupunguza ucheleweshaji wa maamuzi na kuondoa changamoto zilizokuwa zikijitokeza hapo awali.
Aidha, alisisitiza kuwa maboresho hayo yamezingatia maoni ya watumiaji wa awali wa mfumo huo, jambo linalotarajiwa kuongeza usahihi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi za umma.
Kwa upande wao, washiriki wa kikao hicho walipongeza juhudi za Serikali katika kuendeleza mifumo ya kidijitali, wakieleza kuwa hatua hiyo ni chachu ya mageuzi ya kiutendaji na uwazi katika sekta ya umma. Waliahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha mfumo huo unatumika kikamilifu na kuleta matokeo yenye tija kwa Taifa.
Kikao hicho ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kuimarisha utawala bora, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha usimamizi madhubuti wa mali za umma kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa na mifumo jumuishi ya kidijitali.

