Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda , akizungumza Aprili 22,2026, Jijini Dodoma,wakati wa Uzinduzi wa Program ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi jijini Dodoma, ambapo amesisitiza kuwa VETA kupitia urasimishaji ujuzi inampa kijana hadhi na kumfungulia milango ya fursa mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma
Programu ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi imezinduliwa rasmi ikiwa na lengo la kuwawezesha vijana wenye ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi kutambuliwa na kurasimishwa, ili kuongeza fursa za ajira ndani na nje ya nchi.
Aidha, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesisitiza kuwa ujuzi ni mali, mtaji na nguvu ya taifa, na hivyo ni muhimu kwa vijana kujitokeza ili kutathminiwa na kurasimishwa.
Ameyabainisha hayo Aprili 22,2026, Jijini Dodoma, alipokuwa akizindua Programu ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi
Amesema kuwa kupitia programu hiyo ya Mama Samia, serikali inatambua kwamba kumpa kijana cheti cha ufundi stadi siyo tu kumpa karatasi, bali ni kumpa hadhi, sauti na nafasi ya kushindana katika soko la ajira.
Ameongeza kuwa programu hiyo inatekelezwa kimkakati ili kuhakikisha mafundi hawalazimiki kusafiri umbali mrefu, kwani huduma zitawafikia walipo, na kwamba anachotakiwa fundi ni kuwasilisha maombi kupitia ofisi za Halmashauri au vyuo vya VETA vilivyo karibu.
Aidha, amesisitiza kuwa programu hiyo imefadhiliwa kikamilifu na serikali, hivyo hakuna fundi atakayelazimika kulipia gharama yoyote katika mchakato wa urasimishaji ujuzi.
Ameongeza kuwa waajiri wanapaswa kuwa tayari kushirikiana na vijana watakaopata vyeti kupitia mpango huo, ambao unalenga kukuza ajira na ujuzi rasmi nchini.
Aidha, amebainisha kuwa vyeti vinavyotolewa kwa kundi hilo la vijana vinatokana na umahiri wao na vigezo vilivyowekwa na VETA, kupitia miongozo ya kitaaluma.
Pia, Amesema kuwa si kila mwenye ujuzi anarasimishwa moja kwa moja, bali hufanyiwa tathmini, na endapo kuna mapungufu husaidiwa kwa mafunzo ya ziada ili kukidhi viwango vinavyotakiwa.
Ameongeza kuwa cheti cha VETA kinatambulika rasmi na kinampa mhitimu nafasi ya kuaminika katika soko la ajira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amebainisha kuwa lengo la programu hiyo ni kuwafikia wananchi 80,000 kufikia mwaka 2027.
Ameongeza kuwa kwa mwaka huu pekee, serikali imelenga kuwafikia wananchi 30,000, ambapo tayari imepatiwa fedha kwa ajili ya kuwafikia wananchi 14,400 bila malipo yoyote kwa wanufaika.
Amesema kuwa serikali imetoa takriban shilingi milioni 600 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hiyo, na kwamba baada ya kukamilisha awamu ya kwanza, wataendelea na waliobaki ili kufikia lengo lililowekwa.
Pia, Ameongeza kuwa programu hiyo itaongeza ajira na fursa mbalimbali kwa wananchi baada ya kupata vyeti vinavyotambulika rasmi.





