Na Mwandishi Wetu
Miongoni mwa jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika moja kwa moja na fursa zinazotokana na miradi ya kimkakati na uwekezaji kupitia dhana ya Local Content.
Hapo awali, miradi mikubwa ya kimkakati ilitajwa kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa taifa, lakini manufaa yake kwa wananchi wa kawaida hayakuonekana moja kwa moja. Hata hivyo, hali hiyo sasa inabadilika kufuatia jitihada za makusudi za Serikali zinazolenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika miradi hiyo.
Kupitia sera na mikakati mbalimbali, Serikali imeweka mazingira rafiki ya kuwapa Watanzania kipaumbele katika zabuni, ajira, uwekezaji, matumizi ya teknolojia na manunuzi ya umma, ili kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na rasilimali na miradi inayotekelezwa nchini.
Aidha, mikataba ya sekta mbalimbali imeendelea kubainisha wazi wajibu wa kushirikisha Watanzania katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hatua inayochochea matumizi ya nguvu kazi ya ndani na kukuza makampuni ya wazawa.
Mwaka 2025, Serikali iliipa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi jukumu la kisheria kupitia marekebisho ya Sheria ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (Sura 386), ili kuratibu, kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati na uwekezaji nchini.
Hatua hiyo imelenga kuhakikisha kuwa ushiriki wa wananchi unakuwa wa kweli, wenye tija na unaochangia moja kwa moja maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi. Sambamba na hilo, sheria mbalimbali zimeendelea kuimarisha ushiriki wa wazawa, zikiwemo Sheria ya Madini, Petroli, Ununuzi wa Umma, na nyingine zinazohimiza matumizi ya rasilimali za ndani.
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) za mwaka 2024/2025, makampuni ya ndani yalipata zabuni 166,098 sawa na asilimia 99.77 ya zabuni zote, huku makampuni ya nje yakipata zabuni 379 tu sawa na asilimia 0.23. Hii inaonesha kuongezeka kwa ushiriki wa wazawa katika mnyororo wa thamani wa manunuzi ya umma.
Vilevile, vikundi maalum vimenufaika kupitia sera ya kutenga angalau asilimia 30 ya zabuni kwa wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu. Hatua hii imeongeza fursa za kiuchumi kwa makundi yaliyokuwa nyuma kiuchumi kwa muda mrefu.
Katika sekta ya ujenzi, takwimu za Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) zinaonesha kuwa kati ya wakandarasi 1,669 waliosajiliwa mwaka 2024/2025, jumla ya 1,628 ni wazawa. Pia, kati ya miradi 5,330 iliyotekelezwa, asilimia 97.1 ilisimamiwa na wakandarasi wa ndani, hali inayoonesha kukua kwa uwezo wa ndani.
Kwa sasa, Tanzania inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Reli ya Kisasa ya Mwendo Kasi (SGR), Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere Hydropower Project, pamoja na bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ambayo yote imefungua fursa kubwa za ajira na biashara kwa Watanzania.
Kwa mujibu wa taarifa ya NEEC ya Mei 2025, kati ya watu 65,460 waliopata ajira katika miradi mikubwa, asilimia 94 walikuwa Watanzania, jambo linalothibitisha kuongezeka kwa ushiriki wa wananchi katika uchumi wa nchi yao.
Akizungumzia mafanikio hayo, Kaimu Katibu Mtendaji wa NEEC, Bw. Gwakisa Bapala, alisema lengo la Serikali ni kuona Watanzania wanakuwa washiriki wakuu wa uchumi wao badala ya kuwa watazamaji. Alisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa zilizopo katika ajira, biashara na uwekezaji.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto zikiwemo ubora wa baadhi ya huduma na bidhaa za ndani, uelewa mdogo wa fursa zilizopo pamoja na uhitaji wa kuongeza ushirikiano wa kibiashara wenye tija.
Serikali, kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo TANESCO, Tanzania Railways Corporation, TANROADS na nyingine, inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo ili kuhakikisha Watanzania wananufaika kikamilifu na rasilimali na miradi ya maendeleo ya nchi yao.




