Baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita katika shule ya sekondari Agustivo wilayani Mbinga,wakimsikiliza Mkurugenzi wa shule hiyo Joseph Mdaka Mapunda wakati wa mahafali a 16 yaliyofanyika shuleni hapo.

Mkurugenzi wa shule ya sekondari Agustivo Joseph Mdaka Mapunda, akizungumza na wanafunzi,wazazi na walimu wakati wa mahafali ya kidato cha sita ya shule hiyo.

Meneja wa CRDB Tawi la Mbinga Mkoani Ruvuma Beda Mwenda,akikata keki maalum wakati wa mahafali ya kidato cha sita katika shule ya sekondari Agustivo jana,kulia Mkurugenzi wa shule hiyo Joseph Mdaka na wa pili kushoto Mkuu wa shule Moses Mapunda.

Mkurugenzi wa shule ya sekondari Agustivo iliyopo wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Joseph Mdaka,akipokea kipande cha keki wakati wa mahafali a kidato cha sita ya shule hiyo.

Mkuu wa shule ya sekondari Agustivo Moses Mapunda, akipokea zawadi kutoka kwa meneja wa CRDB Tawi la Mbinga Beda Mwenda,wakati wa mahafali ya kidato cha sita jana,katikati Mkurugenzi wa shule Joseph Mdaka Mapunda.

…………..

Na Mwandishi Wetu, Mbinga

WAZAZI na walezi wametakiwa kutochoka na kutoogapa kuwekeza kwa watoto wao ili wapate elimu bora itakayowasaidia kupata ujuzi,uwezo na maarifa kwani katika ulimwengu wa sasa   elimu inachangia sehemu kubwa kumjenga kujitegemea.

Wito huo umetolewa jana na meneja wa benki ya CRDB Tawi la Mbinga Mkoani Ruvuma Beda Mwenda, wakati wa mahafali ya  kumi na sita ya kidato cha sita  ya shule ya sekondari Agustivo wilayani Mbinga.

Alisema,maendeleo kwa jamii yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na kiwango cha  uwekezaji katika elimu, hivyo ni vema jamii ikawekeza nguvu kubwa katika sekta ya elimu ili kujikwamua na umaskini na kupambana katika soko la ajira.

“Tukumbuke kwamba,kuwekeza katika elimu ni mkakati wa muda mrefu unaohitaji dhamira,subira na kwamba matokeo yake huonekana baada ya muda mrefu wa uwekezaji na faida kwa wazazi mara baada ya mtoto kusoma na kuweza kumsaidia pindi anapofikisha umri wa kujitegemea”alisema Mwenda.

Amewapongeza wazazi na walezi kwa kulipa ada kwa watoto wao ili waweze kupata elimu bora kwani fedha wanazolipa kwa watoto wao hazijapotea kwani kuwekeza kwenye elimu ni jambo zuri ambalo litawalipa kupitia watoto pindi watakapoanza kujiajiri na wengine kuajiriwa.

Aidha,amempongeza Mkurugenzi wa shule hiyo Joseph Mdaka Mapunda kwa wazo la  kuanzisha shule hiyo ambayo tangu ilipoanzishwa mwaka 2009 imetoa watu wengi ambao wanaitumikia nchi yetu katika nafasi mbalimbali ambayo ni matunda ya uwekezaji huo.

Mkurugenzi wa shule hiyo Joseph Mdaka Mapunda,amewashukuru wazazi kwa kumuunga mkono kwenye uwekezaji huo kwa kuleta watoto na kulipa ada kwa wakati jambo lililowezesha shule hiyo kuwa na miundombinu bora ya kujifunzia na kufundishia na hatimaye kufanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani mbalimbali ya kitaifa.

“shule yetu ni ya kidato cha 1 hadi 6,kwa hiyo tunaamini mwanafunzi akitoka hapa basimoja kwa moja anakuwa na sifa ya kwenda chuo kikuu kutokana na matokeo mazuri anayopata,namshukuru Mungu kwenye matokeo ya kidato cha sita wanafunzi wato waliohitimu  katika shule hiyo wamepata  sifa ya kwenda vyuo vikuu,nawaomba sana wazazi muendelee kutuletea vijana wenu”alisema Mdaka.

Awali akitoa taarifa ya shule makamu wa shule  ya Agustivo Mosi Msalali alisema,vijana walioagwa ni 49 ambao walianza kidato cha tano  mwezi Julai 2024 wakiwa 53 kati ya o wasichana 19 na wavulana 34,lakini kutokana na changamoto mbalimbali baadhi yao wamehamishwa kwenda shule nyingine na wngine kwenda vyuo  vya ufundi.

Alisema,kitaaluma shule ina mafanikio makubwa katika mitihani ya ndani ya shule,wilaya,mkoa na  kitaifa  ambapo matokeo mbalimbali yameendelea kuwapa hamasa na kuonesha matumaini bora kwa wanafunzi na wazazi na dira ya shule ni kuhakikisha wanafunzi wanaopata daraja la kwanza wanakuwa wengi zaidi na wachache wa daraja la pili.

Alisema,kutokana na juhudi za Mkurugenzi wa shule,bodi ya shule na wafanyakazi wote,ni dhahiri kuwa wahitimu hao watafaulu mitihani yao  ya Taifa inayotarajiwa kuanza mapema mwezi mei 2026 na kujiunga na vyuo vikuu.

Awali wanafunzi hao katika risala yao iliyosomwa na  Gerald Sondi walisema, katika kudumisha taaluma darasa lao limefanikiwa kufanya vizuri katika midahalo ya kitaaluma na michezo mbalimbali na wamegawanyika katika michepuo ya sayansi na Sanaa.

Alisema,katika jitihada za masomo  wamefanikiwa kuunda makundi mbalimbali kwa ajili ya mijadala ya masomo ambayo yamewaongezea ujuzi katika kujibu maswali kwa umahiri na kufanikiwa mitihiani mbalimbali ya ndani na nje.