Mkuu wa Shule ya Sekondari Korona, Mwalimu Christopher Malamsha akizungumza kwenye mahafali hayo jijini Arusha.

Afisa Elimu Sekondari wa Jiji la Arusha, Mwalimu Joshua Mange akizungumza kwenye mahafali jijini Arusha.

Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo,Leon Malisa akizungumza kwenye mahafali hayo jijini Arusha.
………..
Na Happy Lazaro, Arusha
SHULE ya Sekondari Korona iliyopo jijini Arusha imeendelea kufanya vizuri kitaaluma tangu kuanzishwa kwake,huku ikiwa na rekodi ya kutokuwa na wanafunzi waliowahi kupata daraja sifuri.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkuu wa Shule ya Sekondari Korona, Mwalimu Christopher Malamsha, katika Mahafali ya Saba ya Kidato cha Sita yaliyofanyika shuleni hapo ambapo jumla ya wanafunzi 192 walihitimu na kutunukiwa vyeti.
Malamsha amesema kuwa ,mahafali hayo ni ya kihistoria tangu shule hiyo ilipoanza kutoa kidato sita cha kwanza mwaka 2020 yalikuwa hayajawahi kufanyika, ambapo sasa wahitimu wanafuraha kujiandaa kujiunga na vyuo vikuu.
“Tunaendelea kujivunia matokeo mazuri kila mwaka ambapo kwa mwaka jana tulikuwa na watahiniwa 387 ambapo hakuna aliyepata daraja la sifuri, wanafunzi 70 walipata daraja la kwanza na zaidi ya 210 daraja la pili,” amesema Malamsha.
” Mwaka jana hakuna watahiniwa waliopata daraja sifuri. wanafunzi 70 walipata daraja la na zaidi ya 210 daraja la pili,” amesema Malamsha.
“Shule yetu tunafundisha masomo ya PCM na CBG ambapo kuanzia julai mwaka huu tunaongeza masomo mengine ya PCB na PGM na hii yote ni kutokana na kiwango kikubwa cha ufaulu kwa wanafunzi wetu.”amesema Malamsha .
Aidha Malamsha amewataka wanafunzi hao kuhakikisha wanakuwa chachu ya kuleta mabadiliko katika jamii kulingana na yale yote waliyojifunza ikiwemo swala la ujasiriamli ambao wamekuwa wakifanya wakiwa shuleni hapo hali ambayo itawawezesha wao kuweza kujiajiri pindi watakapomaliza masomo yao.
Naye Afisa Elimu Sekondari wa Jiji la Arusha, Mwalimu Joshua Mange, amesema serikali imeanza kuchukua hatua za kushughulikia changamoto mbalimbali zilizobainishwa na wanafunzi pamoja na uongozi wa shule hiyo.
Mange ametaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na miundombinu duni, upungufu wa walimu katika baadhi ya masomo mapya, huduma za afya kwa wanafunzi pamoja na hali ya barabara inayoelekea shuleni hapo.
“Changamoto hizi tumezipokea na tutazifanyia kazi kupitia mifumo rasmi ya serikali ili kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu,” amesema Mange.
Amefafanua kuwa suala la barabara tayari litaingizwa katika vikao vya maendeleo kuanzia ngazi ya kata hadi baraza la madiwani ili lipewe kipaumbele kulingana na upatikanaji wa rasilimali.
Akizungumzia kuhusu upungufu wa walimu, amesema masomo kama Historia, Maadili ya Jamii, Tanzania na Communication Skills yana uhaba wa wataalamu kutokana na maboresho ya mitaala ya hivi karibuni, lakini serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuongeza walimu wenye sifa katika maeneo hayo.
Aidha, amebainisha kuwa tathmini ya mipaka ya shule tayari imefanyika na kubaini haja ya kulipa fidia katika baadhi ya maeneo ili kulinda ardhi ya shule dhidi ya uvamizi, huku hatua za kuingiza suala hilo kwenye bajeti zikiendelea.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo,Leon Malisa ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha kuwa wanahudhuria kwa wingi vikao pindi wanapoitwa mashuleni kwa ajili ya kujadili maendleleo ya watoto wao pampja na kufanya maboresho mbalimbali ya elimu .
“Kumekuwepo na changamoto ya wazazi kutoshiriki vikao shuleni ambapo wakiitwa kwenye vikao wanaojitokeza ni wachache sana jambo ambalo halitakiwi kabisa kwa mustakabali wa wanafunzi wetu ,hivyo wazazi nawaombeni sana mnatakiwa shuleni mjitokeze kwa wingi kwa ajili ya kujadili maendeleo mbalimbali ya shule yetu.”amesema Malisa.




