Na Mwandishi Wetu, Katavi
Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo unaotekelezwa wilayani Mlele, mkoani Katavi, umeanza kuonesha matokeo chanya, huku mashamba darasa ya kilimo na malisho ya mifugo yakigeuka kivutio kikubwa kwa wakazi na wataalamu wa ndani na nje ya nchi.
Aprili 20, 2026, ujumbe wa wataalamu kutoka Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) Kanda ya Kusini mwa Afrika, Taasisi ya Kimataifa ya Urekebishaji wa Maendeleo Vijijini, Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo kutoka Uingereza pamoja na Taasisi ya Teknolojia ya Maendeleo ya Jamii kutoka Zimbabwe walitembelea mashamba hayo kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu.
Ziara hiyo ilihusisha pia wataalamu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wakiongozwa na Mratibu wa Mradi, ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali, Dkt. Zainabu Shaban Bungwa.
Katika ziara hiyo, wageni walitembelea mashamba darasa ya mbegu bora za karanga na mahindi yanayosimamiwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), pamoja na mashamba darasa ya malisho ya mifugo chini ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI).
Mashamba hayo yaliyopo katika vijiji vya Masigo, Utende na Inyonga yameelezwa kuwa mfano wa kuigwa kutokana na usimamizi bora, ubora wa mazao na mwitikio mkubwa wa wananchi. Wageni walivutiwa na namna teknolojia bora za kilimo na ufugaji zinavyotekelezwa kwa vitendo na kuleta tija kwa jamii.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, mtafiti wa TARI, Bi. Caroline Sichale, alisema mashamba darasa hayo yameanzishwa kupitia vikundi vya wakulima na wafugaji kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kipato kupitia matumizi ya mbegu bora na mbinu za kisasa za kilimo.
Kwa upande wake, Mratibu wa shughuli za mradi kutoka FAO Kanda ya Kusini mwa Afrika, Bi. Winnifred Nalyango, aliipongeza Tanzania kwa utekelezaji wa mradi huo, akisema umeonyesha mafanikio makubwa na kuwa mfano wa kuigwa katika nchi nyingine za Afrika.
“Kilichofanyika hapa ni cha kuvutia sana. Mradi huu umeleta mabadiliko chanya kwa jamii na unaweza kuigwa na nchi nyingine,” alisema Nalyango.
Naye Mratibu wa Mradi, Dkt. Bungwa, aliwashukuru wakazi na vikundi vilivyoshiriki pamoja na watafiti kutoka TARI na TALIRI, akiwataja pia wataalamu wa kilimo na mifugo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mlele kwa mchango wao mkubwa, hususan Dkt. Chota wa TALIRI katika kuanzisha na kuendeleza mashamba darasa ya malisho ya mifugo.
Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo unatekelezwa katika mikoa ya Katavi na Tabora, ukihusisha wilaya za Mlele, Urambo, Sikonge na Kaliua, ukiwa na lengo la kuunganisha uhifadhi wa misitu na maendeleo ya kiuchumi kwa jamii zinazozunguka rasilimali hizo.





